Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Ban aipongeza Sri Lanka kwa mwaka mmoja wa kipindi cha mpito

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amempongeza Rais wa Sri Lanka, Maithripala Sirisena, serikali na watu wa nchi hiyo kwa kutimiza mwaka mmoja wa serikali ya mpito wa kisiasa.

Ban ametiwa moyo na serikali kujidhatiti katika ajenda ya mabadiliko  ambayo yana lengo la kuhakikisha amani ya kudumu , utulivu na mafanikio kwa watu wa Sri Lanka.

Katibu mkuu anatambua hatua za awali zilizochukuliwa na serikali kuimarisha utawala bora, hatua za awali za maridhiano na utekelezaji azimio la baraza la haki za binadamu la Oktoba 2015.

UM wakaribisha kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi CAR

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR Parfait Onanga-Anyanga amekaribisha tangazo la matokeo ya Uchaguzi wa rais na wabunge yaliyotangazwa leo nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo na idara ya operesheni za kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, imesema kwamba bwana Onanga-Anyanga amepongeza wagombea Anicet Georges Dologuélé na Faustin Archange Touadéra, ambao wameongoza kwenye awamu hii ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika tarehe 30 mwezi uliopita.

UN Photo/Iason Foounten

Kobler alaani mashambulizi ya kigaidi Libya

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Martin Kobler amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea leo dhidi ya kituo cha mafunzo ya usalama mjini Zliten.

Bwana Kobler ambaye pia ni mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNSMIL ameeleza kushtushwa sana na shambulio hilo. Ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga na kuwatakia nafuu waliojeruhiwa.

Ameongeza kwamba tukio hilo linalochukiza ni ishara ya umuhimu wa kuunda serikali ya mwafaka wa kitaifa na kufufua vikosi vya usalama nchini humo.

China kufunga machimbo ya makaa ya mawe kudhibiti uchafuzi wa hewa

Mamlaka ya taifa ya nishati nchini China, NEA haitoidhinisha machimbo mapya ya makaa ya mawe nchini humo ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo, ikiwa ni  hatua za kudhibiti utoaji wa gesi chafuzi.

Katika taarifa iliyotolewa leo, mamlaka hiyo imesema pamoja na  hatua hizo,  machimbo mengine zaidi ya 1,000 yanayofanya kazi sasa yatafungwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na hivyo kupunguza uzalishaji wa makaa ya mawe kwa asilimia 70.

Walinda amani wa UNAMID waviziwa, wapokonywa silaha

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, UNAMID, umesema kuwa msafara wake wa walinda amani umeviziwa leo na kikundi chenye silaha kisichojulikana, ambapo mlinda amani mmoja amejeruhiwa na silaha kupokonywa.

Tukio hilo limetokea karibu na eneo la Anka, Darfur Kaskazini, mwendo wa takriban kilomita 55 kaskazini mwa mji wa Kutum.

Washambuliaji hao ambao walikuwa wengi zaidi kuliko walinda amani wa UNAMID, pia wameteka mashingani moja, pamoja na bunduki kadhaa na raundi za risasi.

Bei za vyakula zimeshuka kwa mwezi Disemba:FAO

Shirika la chakula na kilimo FAO limesema bei za bidhaa za chakula zimeshuka kwa mwaka wa nne mfululizo mwaka jana kwa wastani wa asilimia 19.1 kutokana na kuyumba kwa uchumi kimataifa hali ambayo imechangia pia kushuka kwa bei za chuma na soko la  nishati duniani.

Kwa mujibu wa FAO miongoni mwa bidhaa zilizoathirika zaidi na kushuka kwa bei ni nyama, bidhaa zitokanazo na maziwa na nafaka , lakini pia sukari na mafuta ya mboga viliguswa.

Ukuaji uchumi duniani kudhoofika, lakini hali shwari: Ripoti

Ukuaji dhaifu wa uchumi katika nchi zinazoibuka kiuchumi utakuwa na madhara katika ukuaji wa uchumi duniani kwa mwaka huu wa 2016.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwezi huu ya Benki ya dunia kuhusu matarajio ya uchumi duniani.

Hata hivyo ripoti imesema licha ya hali hiyo, kasi ya ukuaji uchumi duniani itaongezeka na kuwa asilimia mbili nukta tisa ikilinganishwa na asilimia Mbili nukta Nne mwaka jana kutokana na nchi tajiri kushika kasi kiuchumi.