Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

UNAMID yahimiza utulivu kufuatia hali tete Darfur Magharibi

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika Darfur, UNAMID, umeeleza kutiwa hofu na hali tete inayoendelea katika mji wa El Geneina na karibu na kijiji cha Mouli, yapata kilomita 15 kutoka El Geneina, Darfur Magharibi. Kwa mantiki hiyo, UNAMID imetoa kwa mamlaka za serikali kufanya juhudi zote kuidhibiti hali.

Taarifa ya UNAMID imesema kuwa hali hiyo tete imeibuka kufuatia kikundi kisichojulikana kukivamia kijiji cha Mouli mnamo Januari 9 2016, na kusababisha idadi kubwa ya wanakijiji hicho kukimbilia El Geneina.

Watoto wanaokimbia Yemen bila walezi watafuta usalama Somaliland

Zaidi ya watoto 9,500 kutoka Yemen wamekimbia machafuko nchini humo na kutafuta usalama katika jimbo huru la Somaliland nchini Somalia, wakiwa peke yao bila wazazi au walezi, kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR.

UNHCR imesema watoto hao ni miongoni mwa zaidi ya watoto 168,000 ambao wamekimbia machafuko nchini Yemen tangu Machi mwaka huu, kufuatia kuibuka kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, baada ya miaka mingi ya misukosuko ya kisiasa na kiuchumi, na mivutano ya kidini.

Mtandao wa kukodisha baiskeli New York wafikia Milioni 10 mwaka jana

Mpango wa utekelezaji wa hatua kuhusu mabadiliko ya tabianchi, ClimateAction unaofanya kazi kwa ubia na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP umezungumzia mafanikio ya mtandao wa kukodisha baiskeli kwenye jiji la New York, nchini Marekani.

Mtandao huo umemnukuu Meya wa New York, Bill de Blasio akisema kuwa kwa mwaka jana pekee mtandao huo umehudumia watu Milioni 10 kutokana na baiskeli 7,500 zinazokodishwa kwenye jiji hilo, ambapo matumizi hayo ni ongezeko kwa asilimia 24.

Ubelgiji imechangia Euro milioni 2.45 kusaidia wakimbizi wa Palestina:UNRWA

Serikali ya Ubeligiji imetoa mchango wa Euro milioni 2.45 kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa Palestina UNRWA ikiunga mkono shughuli za shirika hilo katika kutoa huduma kwa wakimbizi kwenye maeneo yanayokaliwa ya Wapalestina.

Mchango huo utagawanywa baina ya mradi wa UNRWA wa kusaidia makazi kwenye Ukanda wa Gaza na mpango wa kusaidia programu ya afya ya akili, inayowalenga wasiojiweza kwenye jamii ya Mabedouin Ukingo wa Magharibi.

Ban alaani shambulio dhidi ya hospitali huko Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani shambulio dhidi ya hospitali inayoendeshwa na madaktari wasio na mipaka, MSF huko jimbo la Sa’ada nchini Yemen ambalo limesababisha vifo vya watu wanne.

Mpaka sasa bado haijafahamika ni nani aliyefanya shambulio hilo la Jumapili ambalo pia limesababisha majeruhi kadhaa.

Ban kupitia taarifa ya msemaji wake ametuma rambi rambi kwa familia za wafiwa na wananchi wa Yemen kufuatia shambulio hilo ambalo ni miongoni mwa mashambulio dhidi ya vituo vya afya nchini humo kufuatia yale ya mwaka 2015.

UM watoa dola milioni 7 kwa misaada ya kibinadamu eneo la Ziwa Chad

Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa,  Stephen O’Brien, ameidhinisha utoaji wa dola milioni saba za Kimarekani kutoka mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Dharura, CERF, kwa minajili ya kutoa usaidizi wa kibinadamu katika eneo la Ziwa Chad.

Kuendelea kwa machafuko na athari za kiuchumi na kijamii kutokana na hali mbaya ya usalama katika eneo hilo, zimelazimu zaidi ya raia 50,000 wa Chad kukimbia visiwa vya Ziwa Chad kati ya Julai na Disemba 2015 na kutafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi wa ndani, vijijini na katika wilaya mbali mbali.

CAR: kikosi cha walinda amani cha DRC charudishwa kwao

Kikosi cha walinda amani kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC kilichokuwa kimetumwa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenye Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA kitarudishwa DRC.

Hii ni kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ambaye amezungumza leo na waandishi wa habari mjini New York Marekani, akieleza kwamba maamuzi hayo yamefuatia tathmini zilizofanyika na idara ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za kulinda amani mwezi Novemba kabla kikosi hakijaanza majukumu yake mwezi Disemba.

Ban ahofia mashambulizi ya anga na mapigano Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amesema anatiwa hofu na ongezeko la mashambulizi ya pamoja ya anga , mapigano ya ardhini na uvurumishaji wa makombora nchini Yemen, licha ya wito uliotolewa mara kadhaa wa kusitisha mapigano.

Ban amesema hofu yake kubwa ni hususan mashambuzi ya anga kwenye maeneo ya amakazi ya watu na majengo ya raia mjini Sana’aikiwemo jengo la chama cha wafanyabiashara, ukumbi wa sherehe za harusi na kwenye kituo cha watu wasioona.

Mkuu wa UNESCO alaani mauaji ya Ruqia Hassan mwandishi habari wa Syria

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO bi Irina Bokova, ameelezea hasira yake kufuatia taarifa za kuthibitisha mauaji ya mwandishi habari wa Syria Ruqia Hassan.

Amesema analaani vikali mauaji hayo na kupongeza ujasiri wa mwandishi huyo aliyesimamia haki za binadamu na uhuru mwingine katika mazingira magumu na kupuuzia kampeni za kikatili zinazotumia itikadi kali kukandamiza uhuru binafsi wa kufikiri, kuongea na kutenda.

UN Photo/Iason Foounten

Ban alaani mashambulizi ya kigaidi Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon  amelaani shambulio la kigaidi nchini Libya lilolenga kituo cha polisi mjini Zliten magaharibi mwa nchi.

Taariaf iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu imesema Bwana Ban ameelezea rambirambi zake kwa familia za waliopoteza maisha au kujeruhiwa na kwa watu wa Libya.

Katibu Mkuu pia amelaani mashambulizi  yanayoendelea kutekelezwa na kundi la Daesh na washirika wake karibu na eneo liitwalo Sidra kati mwa nchi. Amelaani hatua hiyo akisema kuwa ina lengo la kupora rasilimali kutoka kwa watu wa Libya