Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

WFP yasaidia raia zaidi ya milioni moja kaskazini mashariki mwa Nigeria

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema kuwa tangu mwanzo wa mwezi huu wa Desemba, limetoa msaada wa chakula au fedha kwa zaidi ya raia milioni moja katika maeneo yenye vita kwa walioathirika katika Kaskazini mashariki mwa Nigeria.  Hii inamaanisha kwamba zaidi ya nusu ya wale wanaohitaji msaada wa kibinadamu kwa haraka sasa wamefikiwa.

Hatua hii inakuja wakati shirika hilo linawasaidia raia katika majimbo ya Borno na Yobe nchini Nigeria ambako takriban watu milioni nne wana uhaba wa chakula.

UNAMI yalaani utekaji wa mwandishi wa habari huko Iraq

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI) umelaani utekaji wa mwandishi wa habari wa Iraq, Bi Afrah Shawqi, na watu wenye silaha wasiojulikana kutoka nyumbani kwake Jumatatu usiku Desemba 26.

UNAMI imeitaja kuwa shambulizi kubwa juu ya uhuru wa kujieleza nchini ikisema kuwa uhuru ni jambo la msingi kwa jamii zote za kidemokrasia na lazima kuheshimiwa wakati wote na katika hali zote.

Ujumbe huo umetoa wito kwa wahusika kumuachilia huru na kwamba mamlaka ya kuchunguza na watakopatikana na hatia sheria kuchukuliwa haraka iwezekanavyo.

Afya ya uzazi ni msingi wa kuepuka VVU na Ukimwi

Afya ya uzazi kwa watoto wa kike na wasichana barubaru ni msingi wa kundi hili kuweza kujichanua na kufikia kiwango cha juu zaidi cha elimu. Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa usawa wa kijinsia ambalo ni lengo namba 5 la ajenda 2030 ya maendeleo endelevu linaweza kufanikiwa iwapo huduma ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike itapatikana bila vikwazo vyovyote.

Kukatwa kwa bomba kuu la maji Damascus, kwakosesha maji mamilioni ya watu

Umoja wa Mataifa ina wasiwasi kwamba wakazi takriban milioni nne katika mji mkuu wa Syria, Damascus na maeneo ya jirani hawana maji tangu Desemba 22 baada ya bomba kuu la kusambaza maji kukatwa .

Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu OCHA inaeleza kuwa vyanzo vikuu viwili vya maji safi ya kunywa vya Wadi barada na Ain-el-Fijah kwa asilimia 70 ya wakazi hao, havifanyi kazi kutokana na kulengwa na miundombinu kuharibiwa.

UM wakaribisha sitisho la mapigano kote Syria

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura amekaribisha tangazo lililotolewa hii leo la kuanza kwa sitisho la mapigano maeneo yote ya nchi hiyo.

Habari zinasema kuwa milio ya risasi na makombora nchini Syria itakoma kuanzia saa Sita usiku hii leo kwa saa za Syria likihusisha vikosi vya serikali na vikundi vilivyojihami nchini humo.

Chuki dhidi ya wageni ikomeshwe: Eliasson

Viongozi kote duniani wametakiwa kuacha hima kuwagawanya watu katika umimi na usisi, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson anayemaliza muda wake wa uongozi mwishoni mwa mwaka huu.

Bwana Eliasson ameshikilia nafasi hiyo ya pili kwa ukubwa katika shirika hilo kwa karibu kipindi cha miaka mitano huku akiwa pamoja na mambo mengine ameshiriki kikamilifu katika majadiliano ya malengo ya maendeleo endelevu yaliyofikiwa mwaka 2015.

Wataalamu wa UM wapongeza Marekani kuondoa sheria baguzi

Kubaguliwa kwa misingi ya rangi au kidini hadi sasa hakujaleta ufanisi wowote kwenye vita dhidi ya ugaidi, wamesema wataalam wawili wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Ahmed Shaheed na Mutuma Ruteere wamesema hayo wakiangazia Marekani ambayo imefuta sheria iliyoanzishwa baada ya shambulizi la mwezi Septemba mwaka 2011 linaloweka vigezo vikali vya kuingia na kutoka nchini humo kwa raia kutoka nchi 25 za Mashariki ya Kati, Asia ya Kusini au Afrika ya Kaskazini, uitwayo NSEERS.

UNESCO yalaani mauaji ya mchapishaji na mwandishi wa habari

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Irina Bokova, ametaka  uchunguzi wa kina kufuatia mauaji ya mchapishaji na mwandishi wa habari Larry Que nchini Ufilipino. Huku akilaani pia mauaji hayo, Bokova ametaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Taarifa hiyo ya UNESCO inasema kuwa mwandishi huyo alipigwa risasi mnamo Desemba 19 katika mji wa Virac katika jimbo la kati la Catanduanes na akafaa Desemba 20 kutokana na majeraha aliyoyapata.

Visa na mikasa vya wahamiaji Marekani, mhamiaji asimulia alivyotiwa nguvuni sehemu ya 2.

Karibu katika mfululizo wa makala makala ya kusisimua kuhusu madhila ya wahamiaji. Mhamiaji kutoka Kenya Mirara Jogu, anasimulia visa na mikasa ikiwamo ubaguzi aliokabiliana nao kwa zaidi ya miaka 20 ambayo ameishi Marekani.

Baada ya kukamatwa na askari kwa kosa la kuvuka kizimba cha kituo cha treni nini kilifuata? Ungana na Joseph Msami katika simulizi hii.

Msaada toka EU wanusuru maelfu ya wakimbizi: WFP

Shirika la mpango  wa chakula duniani WFP, limekaribisha kuendelea kwa usaidizi kati ya Muungano wa Ulaya EU na shirika hilo ambapo wakimbizi na wasaka hifadhi 17,000 nchini Djibouti wamenufaika.

Taarifa ya WFP inasema kwamba wakimbizi hao wamepatiwa fedha tasilimu pamoja na mgao wa chakula .

WFP imeongeza pia kuwa fedha kutoka kamisheni ya Ulaya ya msaada wa kibinadamu na idara ya ulinzi wa raia (ECHO) zimewezesha shirika hilo kutoa fedha taslimu kwa wakimbizi 13,000 kutoka Somalia, Ethiopia na Eritrea.