Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi wa vijijini Kenya kunufaika na mitambo midogo ya nishati

Wakazi wa vijijini Kenya kunufaika na mitambo midogo ya nishati

Pakua

Kampuni ya Powerhive nchini Kenya inayohusika na kuzalisha nishati salama imeingia makubaliano na kampuni ya Enel Green ya italia ili kuweka mitambo ya kusambaza nishati ya umeme kwenye maeneo ya vijijini nchini Kenya.

Kwa mujibu tovuti ya Climate Action inayofanya kazi kwa ubia na shirika la  mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, mitambo hiyo ya kusambaza umeme kwenye eneo dogo inapatiwa nguvu kupitia nishati ya jua ambapo itahusisha vijiji 100, mradi ukigharibu dola Milioni 12 za kimarekani.

Kupitia  ubia huo, Enel Green watachangia asilimia 93 huku Powerhive wakichangia asilimia Saba iliyosalia.

Afisa mtendaji mkuu wa Enel Green Power Francesco Venturini amesema mradi  huo unadhihirisha hatua thabiti za kampuni za kusambaza nishati za kujumuisha uwekezaji, uendelevu na ubunifu.

Idadi kubwa ya mitambo hiyo ya kusambaza umeme inayotumia nishati ya jua itafungwa huko Kisii na Nyamira Magharibi mwa Kenya ikiwa na jumla ya nguvu ya Megawati Moja huku ikisaidia watu Elfu Tisini.

Nchini Kenya ni asilimia 30 ya watu wana nishati ya umeme huku kukiwa na kiwango kikubwa cha watu wanaotumia simu za mkononi, na hivyo kampuni hiyo ya Enel Green Power imesema kusambazwa umeme kutachochea ubunifu wa kuboresha mfumo wa ankara za malipo.

Photo Credit
Bendera ya Kenya.