Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Kabila la watwa nchini DRC wasalimisha mishale 3000

Wanamgambo wa kabila la watwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wamesalimisha mishale 3,000.

Mishale hiyo ilikuwa inatumika kwenye mapigano ya kikabila kati yao ya na jamii wa kabila la wabantu kwenye eneo la Manono lililopo jimbo la Tanganyika.

Msimamizi wa eneo la Manono Pierre Mukamba amesema hatua hiyo ya kusalimisha silaha hizo za kijadi inafuatia mashauriano kati ya ofisi yake na kabila hilo la watwa na tayari silaha hizo zimeteketezwa.

Uchaguzi mkuu Liberia, UN yatuma mwakilishi wake

Duru ya pili ya uchaguzi nchini Liberia imefanyika hapo jana.

Kufuatia kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi wa Rais nchini Liberia, Umoja wa mataifa ambao umekuwa ukishirikiana na nchi hiyo katika kuhakikisha amani na utulivu imemmtuma msuluhishi wake kwenda nchini humo.

Msuluhishi huyo ni Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo ambaye amekuwa akifanya jukumu la upatanishi nchini humo.

UN yapunguza bajeti yake

Bajeti ya umoja wa Mataifa kwa mwaka 2018-2019 yenye kurasa zaidi ya elfu 8 zilizosheheni maelezo ya mipango mbalimbali na takwimu za taasisi hii kubwa zaidi duniani ilipitishwa mwishoni mwa juma na nchi 193 wanachama wa Umoja huo ikiwa na upungufu wa mamilioni ya dola ikilinganishwa na mwaka 2016-2017 unaomalizika. Tuungane na Assumpta Massoi anayetudadavulia zaidi kuhusu kilichomo, kilichoathirika zaidi na matarajio ya baadaye katika kuhakikisha Umoja wa Mataifa unafanya kazi kwa ufanisi na unawajibika kwa nchi wanachama na walipa kodi.

Nuru zaidi yaangazia wakimbizi walioko korokoroni Libya

Harakati za kuhamisha kutoka Libya wakimbizi walio hatarini zaidi zinaendelea chini  ya usimamizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Katika hatua ya hivi karibuni zaidi wakimbizi 162 walisafirishwa kwenye Roma, Italia kwa kutumia ndege mbili.

Miongoni mwao ni wanawake, watu wenye ulemavu na watoto waliokuwa wanashikiliwa mateka wakiwa na hali mbaya zaidi.

UNHCR imesema wanawake watano kati yao wakati wanashikiliwa mateka walijifungua watoto bila usaidizi wa kutosha wa matibabu.

Guterres apongeza hatua kati ya serikali ya Congo na waasi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha hatua iliyofikiwa huko Jamhuri ya Congo baada ya serikali na Frédéric Bintsamou ambaye hujulikana zaidi kama mchungaji Ntumi kutia saini makubaliano ya kusitisha chuki kati yao.

Makubaliano hayo yalitiwa saini mwishoni mwa wiki ambapo Bwana Guterres amesema ni matumaini yake kuwa yatawezesha suluhu ya kudumu na ya amani kwenye mzozo unaoendelea kwenye eneo la Pool.

Kutoka kujifungulia watoto kwenye lori hadi kupata kituo cha afya

Nchini Papua New Guinea, wanawake wamechukua hatua kulinda afya zao. Baada ya safari za kutwa kucha kufuata vituo vya afya vilivyokuwa vinapatikana umbali mrefu, wanawake walishikamana na kusaka usaidizi kutoka Benki ya Dunia ili kuanzisha kituo cha afya kwenye kijiji chao. Hatua hii inaenda sambamba na lengo namba 3 la malengo ya maendeleo endelevu, SDG linalotaka nchi wanachama kuhakikisha kuwa kila mtu ana afya nje na ustawi wake unalindwa. Sasa huko Papua New Guinea,  hali ilikuwa mbaya hadi wajawazito wanajifungulia watoto kwenye lori.

Japan yasaidia kuimarisha ulinzi wa amani

Mkuu wa operesheni za amani mashinani kwenye Umoja wa Mataifa Atul Khare  amesema mradi wa pande tatu unaohusisha Japan, Afrika na Umoja wa Mataifa umezaa matunda katika kuimarisha operesheni za ulinzi wa amani.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Bwana Khare amesema mradi huo unafadhiliwa na Japan na kusimamiwa na Umoja wa Mataifa huku nchi za afrika zikitoa wanajeshi wanaofanyiwa mafunzo ya uhandisi wa kutengeneza vifaa vinavyotumika vitani wakati wa kulinda amani.

(Sauti ya Atul Khare)