Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Malawi ni kinara wa mapitio ya upunguzaji wa hatari za majanga Afrika:UNISDR

Afrika imefungua ukurasa mpya katika harakati zake za utekelezaji wa mkataba wa Sendai kwa ajili ya kupunguza hatari ya majanga. Kinara ni Malawi, ambayo imefanyia tathimini na kuzipitia sera na hatua zake takribani mwaka mmoja baada ya kukumbwa na mafuriko makubwa.

Tathimini ya siku kumi nchini Malawi iliyofanywa na wataalamu watatu kutoka Msumbiji, Afrika Kusini na Zimbabwe mwezi Disemba imezindua mchakato ambao utakamilisha katika miezi ijayo uwasilishaji wa ripoti ya kwanza kabisa barani Afrika ya mapitio rika kuhusu upunguzaji wa hatari ya majanga.

Waliofurushwa makwao Iraq wahaha kwa mapigano zaidi na baridi

Watu wapatao 400,000 nchini Iraq hawana makazi ya kutosha huku wengine 780,000 wakiishi bila bidhaa muhimu za nyumbani na za kuendeleza ubora wa maisha yao wakati huu wa msimu wa baridi kali, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA.

Kwa mujibu wa OCHA, serikali ya Iraq na wadau wa kitaifa na kimataifa wanaoa usaidizi wa vifaa vya kupasha moto mahema, nguo za joto, fedha, mafuta na vifaa vingine vya kuboresha hali ya maisha.

Karen AbuZayd ndiye mshauri wa mkutano wa masuala ya wakimbizi na wahamiaji

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ametangaza leo uteuzi wa Bi Karen AbuZayd wa Marekani kama mshauri maalumu wa mkutano wa kushughulikia wimbi kubwa la uhamaji wa wakimbizi na wahamiaji ambao utafanyika kwenye baraza kuu la umoja wa Mataifa mwezi septemba 2016.

Mshauri huyo maalumu atafanya kazi kwa karibu na vyombo vya Umoja wa Mataifa na kufanya mashauriano nan chi wanachama na wadau wengine hadi wakati wa mkutano huo.

Safari kuelekea mlima Kilimanjaro kwa ajili ya amani

Walinda amani kutoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS katika juhudi za kueneza ujumbe wa amani ulimwenguni na nchini Sudan Kusini walipanga safari kuelekea nchini Tanzania kwa lengo la kupanda mlima Kilimanjaro ili kupandisha bendera ya Umoja wa Mataifa katika kilele cha mlima huo. Safari hii ambayo ni ya kwanza kuwahi kufanyika miongoni mwa walinda amani ilitimia pale ambao bendera ya Umoja wa Mataifa ilipepea kileleni.Ungana na Grace Kaneiya  katika makala ifuatayo.

Ban alaani mashambulizi dhidi ya magari ya vikosi vya Israel

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amelaani mashambulizi ya jana dhidi ya magari mawili ya vikosi vya julinzi vya Israel katika eneo la mashamba ya Sheba’a mashambulizi ambayo Hizbullah imedai kuhusika.

Katibu Mkuu ameelezea hofu yake dhidi ya mashambulizi ya kulipiza kisasi ya vikosi vya Israel kusini mwa Lebanon , eneo ambalo vikosi vya mpango wa Umoja wa mataifa nchini Lebanon UNIFIL vinaendesha operesheni zake.

Wibisono azungumzia kisa cha kung’atuka ufuatiliaji suala la Palestina

Mtaalamu  maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu kwenye maeneo ya wapalestina, Makarim Wibisono amezungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu wadhifa huo ifikapo tarehe 31 mwezi Machi mwaka huu.

Wibisono amesema msingi wa hatua hiyo ni kitendo cha Israeli kumnyima haki ya kutembelea maeneo yanayokaliwa ya wapalestina akisema harakati zake za kuboresha maisha ya wapalestina ambao haki zao zinakandamizwa zimekatishwa tamaa kila mara.

Watu 9 wafariki dunia katika tetemeko la ardhi India na Bangladesh

Watu wapatao tisa wameripotiwa kufariki dunia leo Jumatatu Januari 4, kufuatia tetemeko la ardhi lililolikumba jimbo la Manipur nchini India, na kuathiri pia nchi jirani za Bangladesh na Myanmar, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA.

Miongoni mwa walioripotiwa kufariki dunia katika tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.7 kwenye kipimo cha richa, ni watu wanane nchini India na mtu mmoja nchini Bangladesh, huku watu zaidi ya 100 wakiripotiwa kujeruhiwa, hususan kwa maporomoko ya nyumba karibu mji mkuu wa jimbo la Manipur, Imphal.

UM walaani mashambulio dhidi ya misikiti Babylon Iraq

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Iraq Ján Kubiš, amelaani mashambulio yaliyofanyika dhidi ya misikiti mitatu ya Kisuni kwenye jimbo la Babylon usiku wa kuamkia leo na vitendo vingine vya ghasia.

Mashambulio hayo matatu ni jarikbio la kuongeza mvutano nchini Iraq na kwenye ukanda mzima amesema bwana Kubiš.Akiongeza kwamba walioendesha mashambulizi hayo wanajaribu kutumia hali ya sasa ya kikanda na kudhoofisha umoja wa Iraq na watu wake na wanatimiza matakwa ya magaidi wa ISIL.