Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

UM walaani mauaji ya wanahabari wa Al-Sharqiya, Iraq

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Iraq, Ján Kubiš, amelaani vikali mauaji ya wanahabari wawili wa televisheni ya Al-Sharqiya, katika mkoa wa Diyala nchini Iraq.

Bwana Kubiš amesema mauaji ya Saif Talal na Hassan Al-Anbaki wakiwa wanafanya kazi yao ya kutoa habari kuhusu matukio ya Diyala ni kitendo cha uovu na uoga kilichotekelezwa na watu wasiotaka ukweli usemwe.

Ametoa wito kwa mamlaka ziwakabili hima waliotenda kitendo hicho, na kuwafikisha mbele ya sheria, pamoja na kufanya kila liwezekanalo ili kuwalinda wanahabari wanapofanya kazi yao.

IOM yasaidia baada ya meli kuzama pwani ya Somaliland

Wahamiaji 36 wamekufa maji wakati meli iliyokuwa imebeba wahamiaji 106 , wasomali na Waethiopia  kuzama pwani ya jimbo lililojitenga la Somaliland kaskazini mwa Somalia siku ya Ijumaa, limesema shirika la kimataifa la uhamiaji IOM.

IOM, ikishirikiana na kitengo cha usaidizi kwa wahamiaji Somaliland (MRC) wanausaidia uongozi wa Somaliland kwa kugawa chakula, maji na madawa kwa manusura. Pia wanatoa malori kwa ajili ya kuwahamisha wahamiaji hao kutoka Harasho walikozama hadi miji ya Sanaag na Erigavo ili kupata matibabu.

DRC: watu milioni 7.5 wahitaji usaidizi wa kibinadamu

Watu milioni 7.5 wanahitaji usaidizi wa kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, wakiwa ni takriban asilimia 9 ya idadi ya watu wote nchini humo.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA nchini humo, kuhusu mpango wa misaada ya kibinadamu nchini DRC kwa mwaka 2016.

Majimbo yote ya DRC yameorodheshwa kwenye tathmini hiyo, lakini yale yanayohitaji usaidizi zaidi ni majimbo ya Kivu kaskazini na Kusini, Ituri, Tanganyika na Maniema yaliyoko mashariki mwa nchi.

Umoja wa Mataifa walaani vikali shambulio la bomu Uturuki lililoua 10

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amealaani shambulio la kigaidi alilooliita  la kupuuzwa huko Sultanahmet nchini Uturuki lililosababisha vifo vya watu 10 na kujerhi takribani 15.

Taarifa ya Katibu Mkuu kupitia ofisi ya msemaji wake inasema kuwa Bwana Ban anatarajia kuwa  watakelezaji wa shambulio hilo watafikishwa katika vyombo vya sheria huku akituma rambirambi zake kwa serikali na watu wake pamoja na serikali ya Ujerumani na raia wengine wa kigeni waliuohusishwa na bomu hilo. Amewatakia majeruhi uponyaji wa haraka.

Nepal: Ujumbe wa akiolojia wa UNESCO kuanzisha mbinu kukabili athari baada ya maafa

Tetemeko la ardhi la 2015 nchini Nepal halikuwa tu zahma kubwa kwa binadamu bali pia lilisababisha athari kubwa kwa utamaduni nchini humo likiharibu urithi wa kipekee wa nchi hiyo.

Urithi huo ambao una nafasi kubwa katika maisha ya watu na chanzo kikuu cha pato la utalii utajengwa upya mwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO.

Nyumba 1,000 za wakimbizi zateketezwa kwa moto Sudan Kusini

Kambi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS inayowapa hifadhi raia 48,000 tangu Disemba 2013 kwenye eneo la Malakal imeteketezwa kwa moto, amesema leo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani.

Bwana Dujarric amesema moto huo ambao ulianza jumapili umeshadhibitiwa baada ya kusababisha pia kifo cha mtoto mmoja, watu nane kujeruhiwa na nyumba 1,000 kuteketea. Hadi sasa chanzo cha moto hakijajulikana.

Mahitaji muhimu yafikia walionasa kwenye mapigano Madaya, Syria

Hatimaye msafara wa magari yaliyobeba shehena za bidhaa muhimu za kuokoa uhai wa binadamu walio kwenye maeneo yaliyoshikiliwa huko Syria, umewasili kwenye mji wa Madaya nchini humo.

Shehena ni pamoja na vifaa tiba, vyakula na mablanketi kutoka Umoja wa Mataifa na washirika wake na lengo ni kufikia wakazi 42,000 ambao wameripotiwa kukumbwa na njaa kutokana na eneo lao kuzingirwa na vikosi vinavyounga mkono serikali.

UN Photo/Loey Felipe

Mchakato wa amani Mali bado ni dhaifu: Baraza la Usalama

Leo Baraza la Usalama limejadili hali ya usalama na kibinadamu nchini Mali pamoja na kufuatilia operesheni za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSMA.

Akihutubia kikao hicho, mkuu wa idara ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za kulinda amani, Hervé Ladsous amesisitiza umuhimu wa kutekeleza maazimio ya makubaliano ya amani, akisema utekelezaji wake ukizidi kuchelewa, hasa kwa upande wa utaratibu wa kusalimisha vikundi vilivyojihami, huenda mapigano yataanza upya.

Miaka 6 baada ya tetemeko la ardhi Haiti, changamoto bado nyingi

Kuelekea miaka sita tangu kutokea kwa tetemeko kubwa la ardhi lililoua zaidi ya watu 200,000 nchini Haiti tarehe 12, Januari, 2010, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza mshikamano wake na familia za wahanga.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amemnukuu Katibu Mkuu akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuendelea kusaidia Haiti katika jitihada za kujenga nchi upya, akiongeza kwamba kupata nafuu tena siyo rahisi, raia wengi wa Haiti wakiendelea kukumbwa na changamoto nyingi.

PASADA yaleta nuru kwa mtoto Halima anayeishi na VVU

Harakati za kupambana na Ukimwi zinashika kasi duniani kila uchao. Miongoni mwa harakati hizo ni kuhakikisha watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wanapatiwa dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo. Mathalani hadi Juni 2015 idadi ya wanaopatiwa dawa hizo walikuwa zaidi ya Milioni 15 na laki Nane ikiwa ni nyongeza kutoka Milioni 13 na Nusu mwaka uliotangulia. Hata hivyo watu wanaoishi na VVU wakiwemo pia watoto wanahitaji msaada zaidi ya dawa pekee. Je ni upi? Na unasaidia nini?