Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jarida la Habari

25 Februari 2021

Jaridani hii leo Flora Nducha anamulika teknolojia na hatua ambazo serikali zinapaswa kuchukuliwa ili ziweze kunufaisha kila mtu na zilete maendeleo ya watu. Watunga sera wakiwemo wabunge wana jukumu lao, ni kutoka UNCTAD. Kisha anakwenda Tanzania hususan mkoani Kigoma ambako kilimo hifadhi charipotiwa kurejesha ujana kwa wakulimia, kivipi? Na mwisho ni kule Uganda ambako msichana mmoja anasema ingawa janga la COVID-19 limemwachia kilema cha kutokuwa na mguu lakini katu halitapora ndoto yake ya maisha. Makala tunamulika matumizi ya dawa za kuuawa wadudu kwenye mboga za majani.

24 Februari 2021

Hii leo jaridani tunaanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako wananchi licha ya madhilla wanayopitia mashariki mwa nchi hiyo wanashikamana na wanasaidiana ili angalau kupunguza machungu. Kisha ni suala la mgao wa mlo shuleni ambao sasa umekwenda mrama kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. Huko Amerika ya kati hali ya chakula nayo ni tabu. Makala leo tunamalizia mahojiano yetu na mtaalamu wa lishe huko Njombe mkoani Tanzania kuhusu umuhimu wa matunda mwilini tukizingatia mwaka wa kimataifa wa matunda na mboga mboga.

23 Februari 2021

Hii leo jaridani Flora Nducha anaanzia na ripoti mpya ya shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, ILO ikiangazia majukwaa mapya ya ajira duniani yakiwemo yale ya mtandaoni na faida na changamoto zake. Kisha anakwenda nchini DR Congo ambako kikongwe mmoja amekata tamaa ya maisha baada ya kufurushwa kwake mara tatu. Taarifa nyingine ni kutoka Lebanon ambako theluji pasi kifani yatishia maisha ya wakimbizi. Makala anabisha hodi mkoani njombe nchini Tanzania mtaalamu wa lishe anazungmzia faida za mboga na matunda.

22 Februari 2021

U hali gani siku ya leo Jumatatu Februari 22 mwaka 2021 na mwenyeji wako Flora Nducha anakueletea mada kwa kina akimulika lugha ya mama, kwa kuzingatia kuwa tarehe 21 mwezi Februari ni siku ya lugha ya mama duniani. Katika kutekeleza hilo Grace Kaneiya akiwa Nairobi, Kenya amefuatilia wito kwa watunga sera, waelimishaji na walimu, wazazi na familia kuimarisha dhamira zao katika kuhakikisha elimu kupitia lugha mbali mbali na ujumuishaji kati elimu ili kuibuka kutokana na athari za janga la virusi vya Corona au COVID-19.

Sauti
11'7"

19 Februari 2021

Leo ni Ijumaa na kama ilivyo ada ni mada kwa kina na tunakwenda Darfur nchini Sudan hususan eneo la Khor Abeche ambako hatimaye wiki hii kambi ya Khor Abeche iliyokuwa inatumiwa na walinda amani wa Tanzania katika UNAMID imekabidhiwa rasmi kwa serikali ya Sudan kufuatia kukamilika kwa majukumu ya ulinzi wa aman jimboni humo. Koplo Japhet Chaula, afisa habari wa kikosi cha 13 cha Tanzania, TANZBATT-13 kwenye UNAMID ndiye alikuwa shuhuda wetu katika tukio hilo la wiki hii.

Sauti
12'41"

18 Februari 2021

Hii leo jaridani Flora Nducha anaanza na masuala ya mazingira ambapo ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inasema bado safari ni ndefu kukabili mabadiliko ya tabianchi. Kisha anabisha hodi Msumbiji ambako anaangazia msaada kwa manusura wa dhoruba kali Eloise. Baada ya hapo anakwenda baharí Hindi visiwani Comoro ambako mradi wa shirika la kazi duniani, ILO umeleta ajira za staha kwa wakazi maskini. Makala tunarejea tena Tanzania jijini Dar es salaam kumulika kilimo cha mboga mboga na matumizi ya muarobaini kukabili wadudu waharibifu.

17 Februari 2021

Hii leo jaridani Flora Nducha anaanzia nchini India ambako mwalimu mmoja wa kiume ameshinda tuzo ya Mwalimu Bora Duniani kwa mwaka 2021 kwa mchango wake katika kutumia uwezo wake kuboresha elimu bila kujali kipato chake. Kisha anamulika utoaji chanjo dhidi ya Ebola huko Butembo jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kutokana na mlipuko wa Ebola. Habati ya tatu inatoka huko Sudan Kusini jimboni Jonglei ambako kuna hofu ya baa la njaa. Makala anabisha hodi nchini Tanzania kwa wakulima wa kilimo cha mjini jijini Dar es salaam. Usisahau na mashinani kunani? Basi ungana naye.

Sauti
12'10"

16 Februari 2021

Hii leo jaridani Flora Nducha aanza na ombi la dola milioni 222 kwa ajili ya wakimbizi wa Burundi waliosaka hifadhi nchi jirani za Tanzania, DRC na Rwanda. Kisha ni Burkina Faso ambako huko afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amefika na kujionea hali halisi ya madhila yanayokumba wakimbizi wa ndani waliofurushwa majimbo ya Kusini Magharibi na Kaskazini Magharibi kutokana na ghasia.

Sauti
13'12"

15 Februari 2021

Hii leo jaridani siku ya Jumatatu ni mada kwa kina na tunamulika nafasi ya redio katika jamii ya sasa na jinsi watangazaji walivyokwenda na wakati ili kuhakikisha chombo hicho adhimu kinaendelea kutekeleza majukumu yake. Katika kufanya hivyo tunakutana na Dina Marious wa kituo cha redio cha E-FM nchini Tanzania. Habari kwa ufupi tunamulika Ebola Guinea miongoni mwa taarifa muhimu. Mashinani tunaelekea nchini Kenya! Mwenyeji wako hii leo ni Grace Kaneiya, karibu!

Sauti
10'52"