Wibisono azungumzia kisa cha kung’atuka ufuatiliaji suala la Palestina

Wibisono azungumzia kisa cha kung’atuka ufuatiliaji suala la Palestina

Pakua

Mtaalamu  maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu kwenye maeneo ya wapalestina, Makarim Wibisono amezungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu wadhifa huo ifikapo tarehe 31 mwezi Machi mwaka huu.

Wibisono amesema msingi wa hatua hiyo ni kitendo cha Israeli kumnyima haki ya kutembelea maeneo yanayokaliwa ya wapalestina akisema harakati zake za kuboresha maisha ya wapalestina ambao haki zao zinakandamizwa zimekatishwa tamaa kila mara.

Amesema kupitia mitandao ya kijamii amesikia vilio vya wapalestina waliokuwa na matumaini makubwa ya utendaji wake kwa sababu ya jitihada za kuwalinda na mazungumzo yake ya moja kwa moja na serikali ya Israel lakini..

(Sauti ya Wibisono)

“Mamlaka yangu ni kufuatilia hali ilivyo kwenye maeneo ya Palestina yanayokaliwa. Naweza vipi kutekeleza wajibu huo iwapo ombi langu la kuyatembelea linakataliwa? Kwa hiyo hili ni suala la msingi kwa sababu mamlaka ni mamlaka ya Umoja wa Mataifa. Iwapo kuna mamlaka ya Umoja wa Mataifa ambayo yanakiukwa na nchi mwanachama inapuuza , basi kwa uelewa wangu hilo ni tatizo kubwa.”

Wakati huo huo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amezungumzia hatua ya kutaka kujiuzulu kwa Wibisono akisema kuwa..

(Sauti ya Dujarric)

Katibu Mkuu mara kwa mara anapokuwa ziarani ameweka bayana kuwa ni muhimu kwa kila nchi wanachama kushirikiana na kufanya kazi na mfumo wa haki za binadamu ikiwemo wataalamu huru kuruhusiwa kutembelea au kuzuru kwa mamlaka yao maeneo ambayo wanahitaji kutembelea ili kutimiza wajibu wao na huo ndio unasalia kuwa msimamo wake.”

Photo Credit
Mmoja wa watoto wa kipalestina ambao mustakhbali wao uko mashakani kutokana na maeneo yao kukaliwa. (Picha:UNRWA/Tamer Hamam)