Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: watu milioni 7.5 wahitaji usaidizi wa kibinadamu

DRC: watu milioni 7.5 wahitaji usaidizi wa kibinadamu

Pakua

Watu milioni 7.5 wanahitaji usaidizi wa kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, wakiwa ni takriban asilimia 9 ya idadi ya watu wote nchini humo.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA nchini humo, kuhusu mpango wa misaada ya kibinadamu nchini DRC kwa mwaka 2016.

Majimbo yote ya DRC yameorodheshwa kwenye tathmini hiyo, lakini yale yanayohitaji usaidizi zaidi ni majimbo ya Kivu kaskazini na Kusini, Ituri, Tanganyika na Maniema yaliyoko mashariki mwa nchi.

Katika ufunguzi wa ripoti hii, mratibu mkuu wa maswala ya kibinadamu nchini DRC, Mamadou Diallo, amesema kwamba mzozo wa kibinadamu umesababishwa na matatizo ya kiusalama na ukosefu wa maendeleo, licha ya mafanikio makubwa kwa upande wa kurejesha utulivu na kuimarisha utawala wa sheria.

Aidha Bwana Diallo amesema mahitaji hayo yanaweza kuongezeka kutokana na matokeo ya uchaguzi unaotakiwa kufanyika katika nchi tano miongoni mwa nchi 9 jirani za DRC mwaka 2016 na 2017 na kusababisha mawimbi ya wakimbizi.

OCHA imeeleza kuhitaji dola za kimarekani milioni 690 kwa ajili ya kutimiza mahitaji hayo kwa mwaka 2016 pekee.

Photo Credit
Usambazaji wa chakula nchini DRC. Picha ya OCHA DRC (akaunti ya Twitter)