Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Watoto 60,000 wanakabiliwa na kifo Somalia

Takribani watoto 60,000 wanakabiliwa na kifo nchini Somalia kwa sababu ya kukosa msaada , kwa mujibu wa mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kwenye nchi hiyo ya pembe ya Afrika.

Mtafaruku wa kisiasa, kurejea mara kwa mara kwa ukame na hata mafuriko, inamaanisha kwamba watoto wapatao milioni tano au nusu ya watu wote wa Somalia wanahitaji aina fulani ya msaada.

Umoja wa mataifa unasema, unahitaji dola takribani milioni 900 kwa ajili ya shughuli za msaada, lakini hadi sasa imepokea asilimia mbili tuu ya fedha hizo.

UM walaani mashambulio mawili ya bomu Iraq

Mashambulio mawili ya mabomu kwenye mji mkuu wa Ira Baghdad, siku ya Jumapili yamelaaniwa vikali na Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya watu 70 wamepoteza maisha katika mashambulizi hayo ambayo yametokea karibu na soko kwenye mji wa Sadr. Kundi la kigaidi la ISIL, ambalo pia hujulikana kama Daesh, limekiri kuhusika na uhalifu huo.

Kufuatia mashumbulizi hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake ameelezea kusitisikitishwa na vitendo hivyo vinavyolenga masoko na sehemu za ibada huku akitaka watekelezaji wa uhalifu huo kuwajibishwa kisheria.

Mjumbe wa amani wa UM Leonardo DiCaprio ashinda tuzo ya Oscar

Mcheza filamu nyota wa Marekani na mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa Leonardo DiCaprio ni miongoni mwa washindi wakubwa katika tuzo za Academy mjini Hollywood zilizotolewa Jumapili usiku.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 ambaye labda anajulikana sana kwa kushiriki filamu ya  'Titanic, amejishindia Oscar ya kuwa mwigizaji bora kutokana na ushiriki wake katika filamu ya 'The Revenant.'

Ufadhili mpya wasaidia WFP kutimiza mahitaji ya Wasyria

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limepata ufadhili wa kutosha wa kurejesha misaada ya chakula kwa wakimbizi wa Syria waliopo Jordan, Lebanon, Iraq na Misri hadi mwisho wa mwaka.

Taarifa iliyotolewa leo imeeleza kwamba usaidizi huo umepatikana kupitia ufadhili mpya ulioahidiwa wakati wa kongamano la kimataifaku husu mahitaji ya kibinadamu Syria uliofanyika mjini London Uingereza hivi karibuni. WFP imesema dola milioni 675 zimeahidiwa, miongoni mwao milioni 623 zikiwa zimetolewa na Ujerumani.

Watafiti kuchunguza yasiyojulikana kuhusu virusi vya Zika na mahitaji

Watafiti mashuhuri kutoka taasisi muhimu za afya watakutana katika Shirika la Afya kanda ya Amerika, PAHO, kuanzia kesho Machi Mosi had Machi Pili, ili kujadili mahitaji muhimu katika kuunda ajenda ya utafiti katika mlipuko wa virusi vya Zika, na athari zake kwa afya.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), imesema watafiti hao wanapanga kutambua upungufu uliopo katika maarifa ya kisayansi kuhuru virusi vya Zika, athari zake kwa binadamu na hatma ya afya ya umma kwa mabara ya Amerika.

Mashirika ya kibinadamu yatumia fursa ya sitisho la mapigano kusambaza misaada Syria

Umoja wa Mataifa na wadau wake wanapanga kusambaza msaada wa kibinadamu kwa raia wapatao 154,000 wanaoshi kwenye maeneo yaliyozingirwa nchini Syria wakati ambapo mapigano yamesitishwa kwa muda.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, usaidizi huo utatolewa kwa kipindi cha siku tano zijazo.

Vifaa vitakavyotolewa ni pamoja na vyakula, vifaa vya tiba dhidi ya utapiamlo, madawa, maji, vifaa vya kusafisha maji na kadhalika.

Baraza la haki lichagize wanachama kutekeleza ajenda ya maendeleo:Lykettoft

Rais wa baraza kuu la Umoja wa mataifa Mogens Lykettoft  ameonya dhidi ya mapungufu makubwa tangu kuundwa kwa Umoja wa Mataifa, yakiwemo baa la njaa, mauaji ya halaiki, na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kwenye kikao cha 31 cha baraza la haki za binadamu mjini Geneva pia ameliasa baraza hilo kuchagiza nchi wanachama kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030.

(SAUTI YA LYKETTOFT)

Ban atiwa hofu na uchaguzi Comoro

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Ban Ki-moon amesema anafuatilia kwa wasiwasi maendeleo chini Comoro tangu tangazo la tume ya taifa ya uchaguzi CENI,  la matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais wa muungano wa nchi hiyo na awamu ya kwanza ya  uchaguzi wa magavana wa visiwa vya Comoro Kuu, Anjouan na Mohéli.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imesema kuwa Bwana Ban ameitaka serikali , wagombea, wadau wengine na taasisi husika katika mchakato wa uchaguzi, kujizuia dhidi ya machafuko na kuhakikisha sheria zinatumika.

Baraza la usalama lapitisha azimio la kusitisha mapigano Syria, majadiliano kuendelea juma lijalo

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha kwa kauli moja  azimio la kuidhinisha ukomeshwaji wa machafuko nchini Syria huku juhudi za mazungumzo ya suluhu la mzozo zikisongeshwa.

Baraza la usalama pia limejdalili hali nchini humo ambapo mwakilishi  maaluma wa Umoja wa Mataifa Syria  Staffan de Mistura amehutubia mkutano huo kwa njia ya video kutoka Geneva.

de Mistura ametaka pande kinzani kutii azimio hilo kwa kusitisha mapigano ilikutoa ahueni kwa raia wanaoendelea kuwa wahanga wa machafuko.  Kadhalika ametangaza kuwa majadiliano yataanza tena juma lijalo.