Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kibinadamu yatumia fursa ya sitisho la mapigano kusambaza misaada Syria

Mashirika ya kibinadamu yatumia fursa ya sitisho la mapigano kusambaza misaada Syria

Pakua

Umoja wa Mataifa na wadau wake wanapanga kusambaza msaada wa kibinadamu kwa raia wapatao 154,000 wanaoshi kwenye maeneo yaliyozingirwa nchini Syria wakati ambapo mapigano yamesitishwa kwa muda.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, usaidizi huo utatolewa kwa kipindi cha siku tano zijazo.

Vifaa vitakavyotolewa ni pamoja na vyakula, vifaa vya tiba dhidi ya utapiamlo, madawa, maji, vifaa vya kusafisha maji na kadhalika.

Taarifa ya OCHA imeeleza pia kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kusambaza misaada ya kibinadamu kwa watu karibu milioni 1.7 iwapo pande kinzani za mzozo zitaupa fursa ya kusafiri kwa uhuru na usalama.

Msemaji wa OCHA Jens Laerke ameeleza kwamba Umoja wa Mataifa unaendelea kuziomba pande kinzani za mzozo uhuru wa kusafiri kwenye maeneo yasiyofikika ya Syria na kuacha kuzingira miji ambapo watu wapatao 500,000 wanazidi kuteseka.

Photo Credit
Mjini Aleppo, Syria. Picha ya OCHA/Josephine Guerrero