Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel acheni sera yenu dhidi ya waafrika- UNHCR

Wakimbizi wa Eritrea, Sudan na Egypt wakimbia nchi zao kuelekea nchi jirani ikiwemo Syria. Picha: UNHCR

Israel acheni sera yenu dhidi ya waafrika- UNHCR

Chonde chonde Israel acheni kuwahamishia nchi ya tatu wakimbizi wa Eritrea na Sudan walioko nchini humo. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema hayo , katika wito wake mwingine kwa nchi hiyo ya Mashariki ya Kati wakati huu ambapo imesema raia hao wakiwemo wale wanaoska hifadhi watalazimika waondoke la sivyo watakamatwa na kuswekwa korokoroni maisha.

UNHCR imechukua tena hatua hii baada ya wasaka hifadhi 80 raia wa Eritrea kupatikana huko Roma, Italia kufuatia safari ndefu ya kuhatarisha maisha yao wakikimbia nchi walizopangiwa na Israel.

Wanaume hao walikiri kupatiwa dola 3,500 ili waondoke Israel lakini walichokuta huko walikopangiwa kwenda ni tofauti na matarajio yao na ndio wakaamua kukimbilia Ulaya.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, William Spindler amesema kulazimisha raia wengine zaidi waondoke wakati huu ambapo mateso yameripotiwa kwa wasaka hifadhi na wahamiaji Libya, ni sawa na kuongeza ukubwa wa tatizo.