Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikopo yahatarisha maisha ya wakimbizi wa Syria huko Lebanon

Wakimbizi wa Syria walioko Lebanon. Picha: UNHCR/Video capture

Mikopo yahatarisha maisha ya wakimbizi wa Syria huko Lebanon

Maisha ya wakimbizi wa Syria waliokosaka hifadhi Lebanon yanazidi kuwa hatarini kila uchao, wakati huu ambapo zaidi ya nusu yao ni mafukara.

Hiyo ni kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la wakimbizi, UNHCR, la watoto, UNICEF na lile la mpango wa chakula WFP.

Mashirika hayo kupitia utafiti wao yamesema miaka saba ya vita nchini Syria imefanya raia wengi kushindwa kukidhi mahitaji ya maisha yao na baya zaidi ni wategemezi kwa misaada ya kimataifa ambayo nayo haina uhakika.

Gharama ya maisha imepanda ambapo kila mtu kwa mwezi anahitaji dola 98 ambapo nusu yake inatumika kwenye chakula. William Spindler ni msemaji wa UNHCR huko Geneva Uswisi.

(Sauti ya William Spindler)

“Kukopa fedha kwa ajili ya chakula, huduma za afya au kodi ya nyumba imekuwa jambo la kawaida sana, ambapo wakimbizi 9 kati ya 10 wanasema wanadaiwa. Hii inaonyesha hali ya hatari ambayo inawakabili wakimbizi wa Syria nchini Lebanon.”

Bwana Spindler amesema tegemeo lao ni mikutano ya kimataifa itakayofanyika Paris, Ufaransa na Brussels, Ubelgiji kwa lengo la kuhamasisha usaidizi zaidi wa kibinadamu hususan kwa wakimbizi hao wa Syria walioko Lebanon.