Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto warohigya waliosalia Myanmar wanaishi maisha dhalili- UNICEF

Baum Myaw, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12, akiwa na familia yake katika kambi ya kambi ya wakimbizi wa ndani karibu na Myitkyina nchini Myanmar. Picha: UNICEF

Watoto warohigya waliosalia Myanmar wanaishi maisha dhalili- UNICEF

Kitendo cha kushindwa kuwafikia watoto wa kabila la Rohingya ambao bado wamesalia nchini Myanmar kinatutia shaka kubwa kwa kuwa wanaishi kwenye mazingira ya kusitikisha.

Kitendo cha kushindwa kuwafikia watoto wa kabila la Rohingya ambao bado wamesalia nchini Myanmar kinatutia shaka kubwa kwa kuwa wanaishi kwenye mazingira ya kusitikisha.

Limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF hii leo kufuatia ziara ya msemaji wake huko jimbo la Rakhine nchini Myanmar hivi karibuni.

Marixie Mercado amesema watoto wapatao 60,000 wamenasa kwenye kambi dhalili katikati mwa jimbo hilo la Rakhine wakiwa katika hali mbaya huku ulimwengu ukielekeza zaidi usaidizi wake kwa wakimbizi 655,000 ambao wameingia Bangladesh.

Ametolea mfano kitongoji cha Pauktaw alichotembelea ambacho kinafikika tu kwa boti akisema makazi yamejengwa juu ya taka, watu wanateka maji kwenye dimbwi la maji yaliyochanganyika na majitaka ya chooni. Kama hiyo haitoshi watoto wanatembea peku.

Bi. Mercado amesema na kule ambako hawawezi kufika….

(Sauti ya Marixie Mercado)

“UNICEF na wadau wake bado hatuna taswira halisi ya watoto waliosalia kaskazini mwa jimbo la Rakhine kwa sababu hatuwezi kuwafikia. Tunachofahamu sasa ni kwamba hali inasikitisha. Kabla ya tarehe 25 mwezi Agosti mwaka jana tulikuwa tunatibu watoto 4,800 waliokuwa na utapiamlo uliokithiri; watoto hawa sasa hawapati tena tiba ya kuokoa uhai wao.”

Amesema wao wako tayari kushirikiana na serikali ya Myanmar na mamlaka za jimbo la Rakhine ili kuwasilisha misaada ya kiutu kwa watoto bila kujadli kabila, dini au hadhi yao na jambo la msingi ni kuweza kufika eneo hilo.