IOM na Zambia wajenga kituo cha mpito kwa wasaka hifadhi mpakani
Nchini Zambia, shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM kwa kushirikiana na serikali wanajenga kituo cha kuhifadhi wahamiaji walio hatarini zaidi kwenye mpaka wa nchi hiyo na Namibia.
Kituo hicho kitapokea wahamiaji na kuwapatia hudukma muhimu kama vile za afya wakati wakisubiri kurejea nyumbani.
Miongoni mwa wahamiaji hao ni wale wanaokuwa wamenusurika kwenye biashara haramu ya binadamu, wasaka hifadhi, wakimbizi na wengineo wanaokimbia hali ngumu ya maisha inayotokana na sababu nyingi ikiwemo majanga ya asili.
Wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo hicho, Mkuu wa IOM nchini Zambia, Marianne Lane na Waziri wa maendeleo ya jinsia wa Zambia Emerine Kabanshi walizindua mkakati wa kudhibiti usafirishaji haramu.
Mkakati huo unalenga kuwapatia wakazi wa wilaya hiyo ya mpakani elimu kuhusu kule waendako ukipatiwa jina Fahamu kabla ya kuondoka au kwa kiingereza Know Before You Go.
Akizungumzia mkakati huo, mkuu wa IOM Zambia amesema kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu kunahitaji ufahamu na uelewa wa mienendo ya kitendo hicho haramu lakini kwa jamii pia ni lazima wafahamu hatari zinazoweza kutokea na pia waeleweshwe juu ya njia za kuweza kuhama kwa usalama zaidi.