IOM kushirikiana na UNICEF kuokoa watoto wahamiaji Libya

10 Januari 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, limesema linashirikiana na mashirika mengine  ya Umoja wa Mataifa kama UNICEF katika kutafuta ufumbuzi wa suala la wahamiaji hasa watoto wasio na walezi nchini Libya. John Kibego na maelezo zaidi.

(Taarifa ya John Kibego)

Othman Belbeisi ambaye ni mkuu wa IOM nchini Libya amesema hayo akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa ambapo amesema mwaka 2017 dunia ilishuhudia  ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wahamiaji  hasa waafrika wanaosaka hifadhi Ulaya kupitia Libya hivyo kusababisha hali ya sintofahamu kwa mustakabali wa watoto wengi wasiokuwa na walezi.

Alipoulizwa nini mpango wa IOM mwaka huu wa 2018 amesema..

(Sauti ya Othman Belbeisi)

“Tumesaini makubaliano na UNICEF ikiwa ni utekelezaji wa  ushirikiano wetu katika kufuatilia kwa ukaribu zaidi  na pia kutoa usaidizi unaohitajika kwa watoto wasiokuwa na wazazi au walezi, na pia  kupata ufumbuzi na suluhu ya kudumu kwa watoto wahamiaji nchini Libya.”

Na vipi kuhusu wahamiaji wanaoendelea kushikiliwa magerezani nchini Libya?

(Sauti ya Othman Belbeisi)

“Tunaendelea kusaka kufungwa kwa vituo mbalimbali vinavyoshikilia wahamiaji , na kutafuta njia mbadala ya kuwahifadhi wahamiaji  hao na pia kuendelea na utoaji wa misaada katika vituo mbalimbali vilivyopo nje ya mji mkuu Tripoli ili huduma muhimu  ziwafikie wahitaji wote.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter