Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana ndio injini tusiwapuuze- Guterres

Mkutano wa tano wa ushirikiano wa Muungano wa Afrika, AU na Muungano wa Ulaya, EU huko Abidjan. Picha: UM

Vijana ndio injini tusiwapuuze- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehutubia mkutano wa tano wa ushirikiano wa Muungano wa Afrika, AU na Muungano wa Ulaya, EU huko Abidjan na kupazia sauti suala la kuwapatia fursa vijana. Leah Mushi na ripoti zaidi.

(Taarifa ya Leah Mushi)

Bwana Guterres katika hotuba yake hiyo aliyoitoa kwa lugha ya kifaransa na kiingereza amesema maudhui ya mkutano huo yanayolenga vijana na ushirikishwaji wao kwa maendeleo endelevu yamekuja wakati muafaka kwa kuwa..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Vijana ni injini ya jamii zetu, tunapaswa kuwasikiliza. Tunapaswa kuwaweka kwenye kitovu cha mipango yetu ya maendeleo kitaifa na kimataifa. Kusikiliza na kujibu hoja zao ni muhimu kwa minajili ya maendeleo, lakini pia kwa ajili ya kulinda amani na usalama.”

Katibu Mkuu akagusia pia sakata la wahamiaji waafrika huko Libya kuuzwa utumwani na picha zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wakitendewa vitendo dhalimu na hivyo amesema..

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia mkutano wa 5 wa ushirikiano wa nchi za Muungano wa Afrika, AU na Muungano wa Ulaya, EU huko Abidjan, Cote D'Ivoire. (picha:Video capture)
(Sauti ya Antonio Guterres)

 “Uhamiaji unawakilisha pengo lakini fursa za maendeleo. Kila nchi inapaswa kulinda mipaka yake lakini pia inapaswa kuheshimu haki za binadamu kwa mujibu wa sheria za ukimbizi na uhamiaji.

Bwana Guterres amesema suluhu ni ushirikiano wa kimataifa kwa kuweka njia halali za uhamiaji kwa kuwa wahamiaji huleta manufaa kwa nchi wanakotoka na kule wanakokwenda.

Halikadhalika amesema serikali zihakikishe zinaweka mazingira bora kwa wananchi wao kujijengea mustakhbali bora na ustawi.