Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano

Okestra kutoka Venezuela yapigia chepuo amani

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa wiki hii kumefanyika tumbuizo la muziki kwa ajili ya kupigia chepuo amani. Amani japo ni neno lenye herufi tano, bado imesalia kuwa ndoto kwa wakazi wengi duniani wakati huu ambapo watu zaidi ya Milioni 123 wamefurushwa makwao kutokana na mizozo iwe ya kiasili au inayosababishwa na binadamu. Tamasha hilo lilihusisha okestra kutoka Venezuela na kwa yaliyojiri tuungane na Assumpta Massoi kwenye makala hii.

Kuna matumaini ya watoto wakimbizi kupata elimu licha ya hali ya ukimbizini

Nchini Ethiopia, idadi ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini ni zaidi ya 350,000. Miongoni mwao, Shirika la Umoja wa MAtaifa la Kuhudumia wakimbizi UNCHR linakadiria kwamba zaidi ya 100,000 ni watoto wenye umri wa kwenda shuleni. Lakini nusu yao tu wamejiandikisha shuleni.

Kwenye kambi ya wakimbizi ya Kule ilioko nchini Ethiopia, mvulana mmoja ameshikilia majukumu katika kuwafundishia wenzake.

Ungana na Priscilla Lecomte kwenye makala hii.

Umoja wa Mataifa waanza kuondoka Liberia, amani yarejea

Kuna usemi usemao nyota njema huanza kuonekana asubuhi, usemi huu unaonekana kutimia katika taifa lililoko Afrika Magharibi Liberia,  ambalo baada ya kushuhudia vita ya wenyewe kwa wenyewe taifa hilo sasa linaelekea kwenye nuru.

Umoja wa Mataifa kupitia ujumbe wake nchini humo UNMIL umejiandaa kuondoka nchini humo baada ya kuwezesha ulinzi wa amani hatua iliyoambatana na kusaidia vikosi vya usalama kuimarisha amani nchini humo. Ungana na Joseph Msami katika makala itakayokupa undani zaidi.

Redio yaelimisha jamii kuhusu malaria DRC

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Radio washirika Umoja imejitahidi kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa malaria uliokithiri kwenye eneo la Fizi, Kivu Kusini.

Kupitia programu mbali mbali redio hiyo imetoa mafunzo kwa wananchi kuhusu jinsi ya kujikinga na mbu na kuzuia maambukizi ya malaria. Wasikilizaji wamenufaika na mafunzo hayo, kadhalika viongozi wa sekta ya afya hadi visa vya malaria vikaanza kupungua, hii kiwa ni ishara ya umuhimu wa redio katika kuokoa maisha wakati huu dunia ikiwa imeadhimisha siku ya kimataifa ya redio hivi karibuni.

Redio ya Umoja wa Mataifa imechangia kukuza Kiswahili- Abdillahi Zuberi

Leo tarehe 13 Februari ni Siku ya Kimataifa ya Redio Duniani. Leo ni siku maalum pia, kwani Redio ya Umoja wa Mataifa inaadhimisha miaka 70 tangu azimio lililokianzisha chombo hicho adhimu cha kupasha habari na kubadilishana mawazo.

Redio ya Umoja wa Mataifa inatangaza kwa lugha nane, zikiwemo Kiswahili, Kireno na lugha sita rasmi za Umoja wa Mataifa ambazo ni Kiingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kirusi, Kichina na Kihispania.

Redio yatumia lugha asilia kusaidia umma nchini Kenya

Nchini Kenya redio kama ilivyo katika nchi nyingine hutumika kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu wakati wa majanga na kwa kupitia lugha za asili ujumbe umekuwa ukiwafikia walengwa kwa namna rahisi.

Ungana na Geoffrey Onditi wa redio washirika KBC katika makala inayofafanua namna redio inavyotumia fursa ya lugha hizo akusaidia wakati wa majanga.

Radio imetumika sana kupasha habari hususan wakati wa majanga- Mbotela

Umuhimu wa Radio bado ni dhahiri katika mataifa yanaoendelea na hususan wakati wa dharura. Katika ujumbe wa mwaka huu katika kuadhimisha siku ya Radio Duniani ambayo ni Februari 13, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limesema kwamba radio ina mchango mkubwa wakati wa kukabiliana na majanga.

Katika mahojiano yafuatayo kutoka Kenya Geoffrey Onditi wa radio mojawapo ya washirika wetu, KBC, amezungumza na mtangazaji gwiji Leonard Mambo Mbotela, mwenye umaarufu unaovuka mipaka ya Kenya, akimweleza umuhimu wa chombo hiki adhimu.

UNAMID redio na wajibu wake katika mizozo Sudan

Siku ya radio duniani hudhimishwa tarehe 13 Februari kila mwaka, mwaka huu inaaadhimishwa sambamba na miaka 70 ya redio ya Umoja wa Mataifa huku umuhimu wa redio katika majanga ikiwa ni maudhui mwaka huu. Nchini Sudan hususani katika jimbo la Darfur redio ya ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika jimboni humo UNAMID pamoja na mambo mengine inatekeleza wajibu muhimu wa kuzipatia fursa za kushiriki kwenye majadiliano pande kinzani ili kupata amani ya kudumu.

Jinamizi la kukeketwa linanitesa:Keziah

"Nikiona nyembe au vitu vyenye ncha kali nakumbuka nilivyokeketwa”Ni kauli ya manusura wa mila potofu ya ukeketaji kutoka Kenya Keziah Oseko ambaye amekutana na mwandishi wa idhaa hii Joseph Msami kandoni mwa mkutano kuhusu kupinga kitendo hicho.

Mwanaharakati huyo kadhalika amesema kuwa ni wajibu wa jamii kukemea kitendo hicho ili kufanikisha kampeni dhidi ya ukeketaji. Kwanza anaanza kulezea lini hasa alianza harakati hizo.

Mtandao wa kuendeleza uhifadhi wa mazingira vyuoni wazinduliwa Kenya

Mtandao mpya umezinduliwa leo na Shirika la Mpango wa Mazingira, UNEP, ukilenga kujumuisha vitendo vya kutunza mazingira na kukuza uendelevu katika mitaala na miradi ya utafiti ya vyuo vikuu nchini Kenya.

Zaidi ya washiriki 160 wamehudhuria hafla ya kuzinduliwa kwa mtandao huo wa Kenya Green Universities Network jijini Nairobi, ambao ni mkakati wa pamoja wa Kamisheni ya Elimu ya Vyuo Vikuu nchini Kenya (CUE), Mamlaka ya Udhibiti wa Mazingira (NEMA), na Shirika la Mpango wa Mazingira (UNEP).