Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Watoto masikini na mayatima Zimbabwe kufadhiliwa misaada ya maendeleo na UM

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) wiki hii limetiliana sahihi na Serekali ya Zimbabwe, pamoja na mashirika 21 yasio ya kiserekali, maafikiano ya kufadhilia jumuiya za kiraia misaada ya kuhudumia uandikishaji ziada wa watoto masikini na mayatima 350,000, ili waweze kuhudhuria masomo ya skuli za msingi. Vile vile msaada huo unatazamiwa kuwahudumia afya na kuboresha lishe watoto husika.

Naibu KM mpya aahidi usimamizi wa kazi za UM kwa nidhamu za fungamano

Ijumatatu, Februari 05 (2007) Asha-Rose Migiro, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo wa Tanzania aliapishwa rasmi kuwa Naibu KM mpya wa UM. Baada ya Bi Migiro kuapishwa na kutia sahihi waraka za UM alijulishwa na KM Ban Ki-moon na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Naibu KM Migiro aliwaambia wanahabari hawo kwamba atajitahidi kama awezavyo kuziongoza kazi za UM kwa nidhamu iliyoungana, na kwa taratibu zinazoeleweka kwa masilahi na natija za taasisi hii pekee ya kimataifa.

Kesi ya Charles Taylor kuanza mwanzo wa Juni mjini Hague

Stephen Rapp, Mwendesha Mashitaka wa Mahakama Maalumu ya Sierra Leone juu ya Jinai ya Vita aliarifu wiki hii kuwa kesi ya aliyekuwa Raisi wa Liberia, Charles Taylor, inatazamiwa kuanza katika mji wa Hague, Uholanzi tarehe 04 Juni 2007. Taylor alifunguliwa mashitaka yenye kumtuhumu kuhusika na vitendo vilivyokiuka haki za kimsingi dhidi ya raia wa Sierra Leone wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe viliposhtadi.

Umma ulion'golewa mastakimu Usomali kupatiwa makazi mapya

Mashirika sita ya UM, yakijumuika na Shirika lisio la kiserekali la kutoka Uholanzi lijulikanlo kama Baraza la Huduma za Wahamiaji la Kidachi,pamoja na jumuiya za kienyeji ziliopo katika mji wa bandari wa Bosaso, Usomali ya kaskazini wamejumuika kuhudumia mpango maalumu wa majaribio wenye lengo la kuzipatia aila 120 zilizong’olewa makwao baada ya mapigano kufumka, makazi mapya. Vile vile familia 30 nyengine masikini kutoka eneo la Bosaso nazo zitafadhiliwa makazi.