Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM Ban Ki-moon ameliarifu Baraza la Usalama juu ya ziara yake Afrika

KM Ban Ki-moon ameliarifu Baraza la Usalama juu ya ziara yake Afrika

Mapema wiki hii KM Ban Ki-moon alikutana na wajumbe wa Baraza la Usalama, kwenye kikao cha faragha, na walizingatia matokeo ya mazungumzo aliyokuwa nayo KM na viongozi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU) walipokutana kwenye pambizo za Mkutano Mkuu uliofanyika karibuni katika mji wa Addis Ababa, Ethiopia.

Vile vile KM alilihimiza Baraza la Usalama kufuatilia kwa nguvu zaidi suala la Darfur, pamoja na kufuatilia masuala yanayohusu utulivu na amani ya mataifa jirani ya Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Alionya kwamba kupwelewa kwa suluhu ya kuridhisha juu ya masuala haya ni hali inayokwamisha zile huduma za dharura za kimataifa zinazohitajika kunusuru maisha ya mamilioni ya watu waathiriwa. Alisisitiza mzoroto huo haukubaliki kimaadili. KM Ban alionya ya kuwa jamii ya kimataifa haina tena muda wa kupoteza, hasa ilivyokuwa wakazi wa Darfur wameshasubiri kwa kipindi kirefu sana kupatiwa suluhu ya maafa yao na wanahitajia haraka misaada ya kimataifa.

Kadhalika KM aliripoti katika Baraza la Usalama juu ya maendeleo ya karibuni katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Cote d’Ivoire na Usomali.