Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

UM yanuia kukomesha karaha ya utumiaji mabavu dhidi ya wanawake

KM wa UM Ban Ki-moon aliwasilisha risala maalumu, na muhimu, kwenye taadhima za kuiheshimu Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumiaji Mabavu dhidi ya Wanawake. Jumuiya ya Kimataifa iliafikiana kuitambua tarehe 25 Novemba, kila mwaka, kuwa ni siku kuuzindua umma wa dunia juu ya jukumu kuu, na tukufu, la kupiga vita, kipamoja, vitendo karaha vya kutumia mabavu na nguvu dhidi ya watoto wa kike na wanawake.

Manadalizi ya vikosi mseto vya UM/UA katika Darfur yasonga mbele

Kundi la kwanza la wahandisi wa kijeshi 135 kutoka Uchina wamewasili karibuni mjini Nyala, katika Darfur Kusini, wakijumuisha furushi la mchango wa UM kusaidia Operesheni za Umoja wa Afrika za AMIS katika Darfur. Vikosi hivi vya Uchina vitahudumia kazi muhimu ya kutayarisha makazi kwa vikosi mseto vya ulinzi wa amani vya UM na UA vya UNAMID.

John Holmes, Mkuu wa OCHA ameanza ziara ya siku tisa Afrika

Naibu KM juu ya Misaada ya Dharura, John Holmes ameanza ziara ya siku tisa Afrika na alitazamiwa kuzuru Ethiopia, Sudan na Kenya. Holmes atakutana kwa mashauriano na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayohudumia misaada ya kiutu pamoja na maofisa wa UM, na pia wanadiplomasiya waliopo kwenye nchi anazozuru kushauriana juu ya hatua zinazofaa kuchukuliwa shirika, ili kuwanusuru kimaisha mamilioni ya watu walioathirika kihali kutokana na mifumko ya vurugu liliotanda kwenye maeneo yao katika siku za karibuni.

UM umechapisha kitabu cha mwongozo kusaidia vijana wa vijijini Afrika

Mashirika mawili ya UM yanayohusika na chakula na kilimo, FAO, na miradi ya chakula duniani, WFP yamechapisha kitabu kipya cha mwongozo kuwasaidia vijana walioathiriwa na UKIMWI/VVU katika mataifa ya Afrika kusini ya Sahara kuanzisha skuli za ukulima za kuilimisha watoto mayatima ufundi na ujuzi wa ajira ya kudumu. Mafunzo haya vile vile yatwasaidia vijana wanaoishi vijijini Afrika kupata uzoefu wa kudhibiti bora akiba ya chakula kwa muda mrefu, hasa ilivyokuwa wanakabiliwa hivi sasa na mazingira magumu ya kimaisha.

Mtaalamu wa haki za binadamu anakhofia upungufu wa uhuru wa dini Angola

Asma Jahangir, Mkariri Maalumu anayehusika na masuala ya uhuru wa dini na itikadi alizuru Angola karibuni kwa wiki moja. Baada ya kumaliza ziara yake Jahngir aliripoti kwamba licha ya kuwa katiba ya taifa inaruhusu uhuru wa kuabudu na kufuata itikadi za dini mbalimbali kwa raia, aligundua kwamba baadhi ya vikundi vya Kikristo pamoja na jamii ya Kiislamu katika Angola bado wanaendelea kubaguliwa kisheria.

UNMIL kushirikiana na Serikali Liberia kuzalisha ajira

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani Liberia (UNMIL), likishirikiana na Benki Kuu ya Dunia, UNDP, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) na shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) linaendeleza mradi maalumu wa pamoja wa kujenga barabara zilizoharibiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, mradi utakaosaidia kuzalisha ajira kwa watu 50,000 vijijini. Mradi huu unaendelezwa shirika na Serikali ya Liberia, halkadhalika.

Waasi wajisalimisha kwa walinzi wa amani katika JKK

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUC) limeripoti kwamba Micho Bizaboso, kamanda wa cheo cha juu katika kundi la waasi la Jenerali Mtoro, Laurent Nkunda karibuni alijisalimisha kwa vikosi vya UM, yeye pamoja na wafuasi 14 wengine baada ya kushindwa nguvu na wanajeshi wa MONUC.