Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA

LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA
Lugha ya kiswahili kuadhimishwa kimataifa kila tarehe 7 Julai - UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO tarehe 23 mwezi Novemba mwaka 2021 lilitangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu ni Kiswahili kwa amani na ustawi. Lengo hasa la maadhimisho haya ya mwaka ni kusongesha matumizi ya lugha ya kiswahili kama nguzo ya amani, na ustawi na wakati huo kuimarisha tamaduni mbalimbali.

UNESCO ilipitisha uamuzi huo huko makao makuu yake mjini Paris Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo.
Azimio lilipitishwa bila kupingwa na utekelezaji wake unaanza mwaka huu wa 2022.

Kupitia ukurasa huu mahsusi, utapataa taarifa zote kuanzia kupitishwa kwa azimio hilo, mapokeo yake na harakati za kukuza lugha ya Kiswahili ili iweze kujenga amani, uchumi, maendeleo na utangamano katika kona mbali mbali za dunia.

Utapata taarifa zilizochapishwa, video kutoka watu mbalimbali iwe maafisa wa serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, maafisa wa UN wenyewe, wanazuoni, wanafunzi na wananchi wa kawaida.


 

06 OKTOBA 2022

Hii leo katika Habari za UN Assumpta Massoi anakuletea Habari kwa Ufupi, Mada kwa Kina na Kujifunza Lugha ya Kiswahili.

Katika Habari kwa Ufupi kuna haki za mtoto kuzingatiwa hasa wakati huu ambapo majanga ya kiasili na yanayosababishwa na binadamu  yanakengeua utekelezaji wa haki za mtoto. Suala la afya ya akili barani Afrika ambayo inachochea matukio ya kujiua ,na WHO imezindua kampeni maalum. Na kisha ni uzinduzi wa ripoti kuhusu matumizi ya matukio makubwa ya michezo ili kuimarisha afya ya mwili ya binadamu.

Sauti
11'26"

29 SEPTEMBA 2022

Hii leo Alhamisi ni mada kwa kina Flora Nducha anakupeleka nchini Kenya hususan kaunti ya Migoro kumulika changamoto ya elimu hasa maeneo ya vijijini, lakini zaidi ya yote ni kwa vipi elimu sio tu ufunguo wa maisha bali pia msingi wa maendeleo kama usemavyo Umoja wa Mataifa.

Habari wa Ufupi zinamulika ripoti kuhusu nchi 42 kubinya watu kushirikiana na Umoja wa Mataifa kwa kuwapatia vitisho au kulipa visasi. Halikadhalika siku ya kimataifa ya upotevu wa chakula kuanzia shambani hadi mezani na bila kusahau siku ya kimataifa ya usaifirishaji baharini.

Sauti
11'55"
UN

JIFUNZE KISWAHILI : Mzishi

Leo Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi wa Baraza la Kiswahili Taifa Tanzania, BAKITA, anafafanua maana ya neno Mzishi, akisema katika hali ya msiba ndio kuna mzishi. Huyu ni ndugu au jamaa anayeshughulikia mazishi ya mtu. Mzishi anashughulikia mazishi ya mtu na ni mtu ambaye anaweza kuwa karibu na mtu wakati wa shida na raha.

Sauti
52"

30 AGOSTI 2022

Katika jarida la Umoja wa Mataifa hii leo Flora Nducha anakuletea 

-Nusu ya vituo vya huduma za afya duniani kote vinakosa huduma za usafi na hivyo kuwaweka wagonjwa na wahudumu wa afya katika hatari kubwa ya kusambaza magonjwa na maambukizi kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na WHO na UNICEF.

Sauti
12'56"

18 AGOSTI 2022

Hii leo jaridani tuna Habari kwa Ufupi ikianzia Ukraine ambako Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres yuko ziarani na anasema mashirika ya kiraia na taasisi za elimu ya juu ni muhimu zaidi hivi sasa kusongesha demokrasia ya kweli. Kisha tunakwenda Syria huko mtoto ameuawa na kilipuzi alichokuwa akichezea. Na hatimaye Zimbabwe wanaweke nyavu madirishani na milangoni kuzuia mbu.

Sauti
13'29"

12 AGOSTI 2022

Hii leo jaridani tunamulika siku ya vijana tukianza na ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akitaka vijana wajumuishwe na kubwa zaidi mfumo wa elimu urekebishwe. Kisha tunamulika furaha waliyoipata watu wa jamii ya kabila la washona nchini Kenya ambao baada ya kuhamia nchini humo miaka ya 1960 hatimaye wamepata uraia na kuweza kupiga kura. Makala tunamulika Kiswahili na tunakwenda DRC na Ujerumani. Mashinani ni ujumbe kwa vijana. Karibu na mwenyeji wako ni Assumpta Massoi.
Sauti
11'7"