Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano na mjadala siku ya Kiswahili UN kuendeshwa kwa Kiswahili- Prof. Gastorn

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Profesa Kennedy Gastorn akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu siku ya Kiswahili.
UN/ Assumpta Massoi
Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Profesa Kennedy Gastorn akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu siku ya Kiswahili.

Mkutano na mjadala siku ya Kiswahili UN kuendeshwa kwa Kiswahili- Prof. Gastorn

Utamaduni na Elimu

Kuelekea kilele cha maadhimisho ya kwanza ya siku ya kiswahili duniani kesho Julai 7, 2022 uwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa utakuwa na matukio makubwa matatu yatakayofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Profesa Kennedy Gastorn ameieleza Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa tukio la kwanza litakuwa asubuhi kuanzia saa 4 kwenye ukumbi namba 3 wa makao makuu ya  Umoja wa Mataifa, likihusisha hotuba kutoka viongozi wa ngazi ya juu akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na marais na wakuu wa nchi zinazozungumza lugha ya Kiswahili.

Viongozi watatoa matamko kwa lugha ya Kiswahili

“Viongozi wakuu watatoa matamko yao akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, marais kutoka kusini mwa Afrika kama Msumbiji na Zimbabwe, tunatarajia viongozi wa Afrika Mashariki mfano Uganda na Kenya na viongozi wa mashirika makubwa kama Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO,” amesema Balozi Gastorn.

Amesema baada ya matamko ni wakati wa mjadala utakaojikita katika nafasi ya Kiswahili katika amani ya maendeleo. “Wazungumzaji ni pamoja na wanazuoni, watu binafsi, sekta binafsi na viongozi wa serikali.”

Mwakilishi huyo wa kudumu amesema watatoa maoni yao ni kwa vipi kiswahili kimekuwa ni nyenzo ya kuendeleza amani, kuunganisha watu “na katika kuendeleza maisha ya watu tunapoelekea kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGS.”

UN imepitisha azimio la matumizi ya lugha mbalimbali, 'multilingualism' na lugha ya Kiswahili ni miongoni mwao. - Profesa Kennedy Gastorn, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania- UN

Sehemu ya tatu ni maonesho ya mila na desturi za kiswahili ikiwemo mavazi, chakula na nyimbo na hili litafanyika kwenye ofisi za uwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.

“Cha kutia moyo ni kwamba kutakuwepo na watoto wa shule ya awali  kutoka hapa Marekani ambao wanajifunza lugha ya kiswahili . Wataonesha umahiri wao katika kiswahili na hili ni jambo la furaha kama wanavyosema wahenga kuwa ‘ngoma inayodumu ni ile inayochezwa na marika yote’ hivyo uwepo wa watoto wa shule ya awali nje ya mipaka ya Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika ni ishara nzuri kwamba kweli sasa kiswahili kinashika hatamu,” amesema Balozi Gastorn.

Ametanabaisha kuwa kwa mara ya kwanza mkutano na mjadala ndani ya Umoja wa Mataifa utaendeshwa kwa lugha ya kiswahili kwa sababu kutakuwepo na wakalimani wa lugha zote rasmi za Umoja wa Mataifa kutoka lugha ya Kiswahili.

Wanafunzi wa shule ya msingi ya Ngome mkoani Iringa nchini Tanzania wakiwa na makaratasi yameandikwa Kiswahili Kwa Amani.
UN Social Media/Eghbert Bitungwa
Wanafunzi wa shule ya msingi ya Ngome mkoani Iringa nchini Tanzania wakiwa na makaratasi yameandikwa Kiswahili Kwa Amani.

Kiswahili ni fursa ni lugha ya AU, SADC na EAC

Balozi Gastorn amesema kwa wale wanaozungumza lugha ya kiswahili au wenye nia ya kujifunza ni vema wafahamu kuwa Kiswahili ni fursa.

“Hii ni kwa sababu sasa lugha hiyo ni lugha rasmi Muungano wa Afrika, Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika na lugha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na sasa imetengewa siku rasmi kwenye Umoja wa Mataifa.  Na hii ni mwanzo tu, tunatarajia kuwa baadaye lugha hii itakuwa lugha rasmi ya Umoja wa Mataifa,” amesema Balozi Gastorn akiongeza kuwa zaidi ya hayo lugha ni mawasiliano na pia huonesha au husambaza utamaduni wa watu  husika.

Kwa mantiki hiyo amesema wenye lugha ya kiswahili watembee kifua mbele sasa tamaduni zao zinatambulika na zinaenea.

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la matumizi ya lugha mbalimbali ndani ya Umoja wa Mataifa, multilingualism, “kiswahili tayari kimeingia kwenye azimio hilo na hii inadhihirisha kukubalika kwa kiswahili ndani ya Umoja wa Mataifa.”