Kutambuliwa kwa lugha ya kiswahili kimataifa ni tunu ya kipekee- Rais Nyusi

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji akihutubia kwa njia ya video  washiriki wa maadhimisho ya kwanza kabisa ya siku ya Kiswahili duniani, maadhimisho  yaliyofanyika kwenye makao makuu ya UN New York, Marekani.
UN Video

Utamaduni na Elimu

Msumbiji imesema kutambulika kwa lugha ya kiswahili kimataifa ni tunu na heshima kubwa kwa wazungumzaji wote wa lugha hiyo duniani.

Hiyo ni kauli ya Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi katika ujumbe aliotoa leo kwa njia ya video kwenye maadhimisho ya kwanza kabisa ya lugha ya kiswahili duniani, maadhimisho yaliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Maadhimisho hayo yameandaliwa kwa pamoja na ujumbe wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa AFrika, SADC, Jumuiya ya Afrika MAshariki, EAC na wadau wengine kutoka nchi zinazozungumza Kiswahili.

Miongoni mwa washiriki wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani kwenye makao makuu ya UN,  New York, Marekani. Mwaka 2021 UNESCO ilitangaza Julai 7 kuwa siku ya Kiswahili duniani
UN /Manuel Elias
Miongoni mwa washiriki wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani. Mwaka 2021 UNESCO ilitangaza Julai 7 kuwa siku ya Kiswahili duniani

Kiswahili kinakua kila uchao

Rais Nyusi amesema, “Kiswahili ni lugha inayokua kwa kasi sana na yenye umuhimu mkubwa. Kuzungumza Kiswahil ini kurahisisha mawasiliano na kuunganisha watu wa mbalimbali. Kiswahili ni kielelezo cha kipekee cha desturi na utamaduni wetu, ustaarabu pamoja na fikra zetu.”

Ameweka bayana pia nafasi ya lugha ya Kiswahili katika mawasiliano, sayansi na teknolojia akisema, “kiswahili kinatuwezesha kupata habari, elimu, mawazo mapya pamoja na kumiliki sayansi na teknolojia.”

Rais Nyusi pamoja na kunukuu UNESCO kuwa kiswahili lugha ya kibantu yenye chimbuko lake pwani ya AFrika, ni moja ya lugha 10 zinazozungumzwa zaidi duniani, amesema hata nchini mwake Msumbiji lugha hiyo inatumika sana.

UN News/Anold Kayanda
Kiswahili kinazungumzwa sana Msumbiji- Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji

Kiswahili si lugha ya mtaani pekee

“Kiswahili si lugha ya mitaani tu, bali kinatumika bungeni, kinafundishwa katika vyuo mbalimbali duniani, kinasikika kwenye radio, televisheni au runinga,” amesema Rais Nyusi.

Ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa kumpatia fursa ya kutoa salamu za pongezi kwa niaba yake binafsi na kwa ajili ya wananchi wa Msumbiji kwa maadhimisho ya leo.

Baraza Kuu la UNESCO lilipitisha mwezi Novemba mwaka jana bila kupingwa azimio la kutangaza tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.