Lugha ya Kiswahili imeonesha kuwa jumuiya ya kimataifa inaweza kuja pamoja kwa lengo moja - Evariste Ndaishimiye

Rais wa Burundi Evariste Ndayimishiye akihutubia kwa njia ya video maadhimisho ya kwanza ya siku ya kimataifa ya lugha ya Kiswahili kwenye makao makuu ya  UN, New York, Marekani.
UN Video
Rais wa Burundi Evariste Ndayimishiye akihutubia kwa njia ya video maadhimisho ya kwanza ya siku ya kimataifa ya lugha ya Kiswahili kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani.

Lugha ya Kiswahili imeonesha kuwa jumuiya ya kimataifa inaweza kuja pamoja kwa lengo moja - Evariste Ndaishimiye

Utamaduni na Elimu

"Ndugu zangu ulimwenguni kote, kama shahidi katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki, nina uhakika Kiswahili ni lugha yenye uwezo wa kuvuka mipaka." Hivyo ndivyo Rais wa Burundi Evariste Ndaishimiye alivyoanza salamu zake za kuutakia ulimwengu maadhimisho mema ya Siku ya Kiswahili Duniani.

Rais Ndaishimiye kupitia ujumbe wake huo alioutoa kwa njia ya video akionekana mwenye bashasha, ameeleza kuwa lugha ya Kiswahili ni dhahiri imeonesha ni jinsi gani ulimwengu unaweza kuja pamoja kwa lengo moja kama ambavyo suala la Kiswahili limeileta jumuiya ya kimataifa pamoja.

Akijenga hoja yake hiyo ameanza kwa kutoa mfano wa nchini Tanzania ambako kuna lugha nyingi za makabila, lakini watu wote wameletwa pamoja na lugha moja ya Kiswahili na kisha akaenda kimataifa akisema, "lugha hiyo imeonesha kwamba jumuiya ya kimataifa inaweza kuja pamoja na lengo moja. Kiswahili huzungumzwa nchini Burundi, huzungumza nchini Kenya, Uganda, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC hata nchini Rwanda." 

Julai 7 ni siku ya lugha ya Kiswahili duniani
UN
Julai 7 ni siku ya lugha ya Kiswahili duniani

Nchi zote hizo pamoja na nyingine ulimwenguni kwa namna mbalimbali zimeungana kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani ambayo imefanyika leo Julai 7, 2022 kwa mara ya kwanza tangu shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO lilipoitambua lugha ya Kiswahili kimataifa na kuitengea siku rasmi ya kuadhimishwa duniani kote. 

Akikipia chepuo kiswahili, Rais Ndaishimiye amesema, "ni vizuri kuzungumza lugha moja kwa sababu tunaposhiriki mawazo tunakuwa kitu kimoja, tunakuwa na maono sawa, na kufanya kazi pamoja. Hii inatupa matumaini ya wakati bora ujao kwa watu wetu hivyo tuungane tufanye kazi kwa umoja na sauti moja. Shukrani kwa waafrika wote wanaoendelea kudai kuwa Kiswahili kifanywe lugha rasmi ya Afrika."