Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Acheni kutumia lugha msiyofahamu vyema, tumieni Kiswahili- Balozi Mongella

Balozi Gertrude Mongella, akihojiwa na Stella VUzo wa UNIC Dar es salaam (Picha Maktaba)
UN Tanzania/Ahimidiwe Olotu
Balozi Gertrude Mongella, akihojiwa na Stella VUzo wa UNIC Dar es salaam (Picha Maktaba)

Acheni kutumia lugha msiyofahamu vyema, tumieni Kiswahili- Balozi Mongella

Utamaduni na Elimu

Miongoni mwa watu waliopokea kwa shauku kubwa kutambuliwa kwa lugha ya Kiswahili kimataifa ni aliyekuwa Rais wa Bunge la Afrika Balozi Gertrude Mongella kutoka Tanzania ambaye yeye amesema sasa anajivunia kujiita anatoka taifa linalozungumza lugha ya Kiswahili au Swahiliphone badala ya wale waingereza, Anglophone au wafaransa, Francophone.

Balozi Mongella amesema hayo katika mahojiano haya yafuatayo aliyofanya na Stella Vuzo wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC, jijini Dar es salaam nchini Tanzania wakati wa shamrashamra za kuelekea siku ya Kiswahili duniani tarehe 7 mwezi Julai mwaka huu.

Stella Vuzo:  Leo tunasherehekea siku ya Kiswahili duniani, mara ya kwanza kabisa kuadhimishiwa duniani kote! HIi siku ina maana gani kwako?

Balozi Mongella: Hii siku ni ya muhimu sana kwangu, kwa sababu ni siku ambayo inaifanya Afrika na yenyewe iweze kutambulika kuwa watu wa Afrika walikuwa na lugha zao muhimu na zilikuwa zimeendelea. Kiswahili ni lugha ambayo imeeleweka duniani kote, Tanzania na mimi nashukuru ya kwamba ukombozi wa bara la Afrika ulisaidia sana Kiswahili kuvuka mipaka ya Tanzania. Lakini pia kazi ambazo tumefanya katika Umoja wa Afrika na sasa Muungano wa Afrika na katika elimu ya lugha, nadhani imetusaidia sana. Imetusaidia kwa maana watu wengi walikuwa hawajatambua kuwa tunapojiita Francophone au Anglophone tunapoteza utu wetu na kutambulika kwetu. Na mimi kila wakati nilikuwa nashangaa kwa nini watu wa Afrika wajiite Anglophone au Francophone. Na wakati nafanya kazi Bunge la Afrika niliudhika sana na mtu mmoja siku moja kusema kuwa “samahani Mheshimiwa Mwenyekiti unapendelea zaidi watu wanaotoka mataifa yanayozungumza Kiingereza kila mara unawapatia fursa  ya kuzungumza Nami nilimwambia unakosea sana, mimi si Anglophone wala Francophone mimi ni SWahilphone. Na sasa najisikia mimi ni Swahiliphone, lugha ya kiafrika, lugha ambayo inatufanya na sisi waafrika tutambulike.

Tweet URL

Stella Vuzo: Umepokeaje suala la Muugano wa AFriak kukubali kutumia lugha ya Kiswahili kama moja ya lugha za mawasiliano?

Balozi Mongela: Mimi nilitambua hilo mapema sana kwa sababu wakati niombea kazi Umoja wa Mataifa nilikuwa nafahamu Kiswahili, Kiingereza na Kikerewe. Na nilisema hivyo nikiwa na matumaini kuwa iko siku Kiswaihili kitatumika kama lugha ya kufanyia kazi kwenye Umoja wa Mataifa au Muungano wa Afrika. Kwa hiyo tumejikomboa kutumia lugha za waliotutawala, na sasa ni lazima tuendelee kuimarisha lugha za kiafrika kama vile Kiigbo kutoka Nigeria na nyinginezo kwa sababu watu walitambua kiarabu na kwa mwafrika wa kawaida kiarabu si lugha yake bali waliotoka urabuni. Lugha ya Kiswahili imeimarika sana kifasihi na watu hawana sababu ya kutokitambua..

Stella Vuzo: Kwa mtazamo wako Kiswahili kina nafasi gani katika kutumika na viongozi walioko madarakani au kwenye taasisi mbalimbali?

Balozi Mongela: Kina nafasi kubwa kwani fasihi yake imeendelea sana. Pili kina nafasi kubwa kwa kuwa lugha nyingi hasa za kibantu mashina yake yametokana na lugha ya kiswahili na lugha nyingi za kiafrika zina msingi wa kibantu kutoka kusini mwa Afrika. Kwa hiyo haitatupa matatizo . Kwa viongozi nadhani si tatizo ukiangalia hata kiingereza chenyewe tunajiuma uma. Kifaransa halikadhalika. Tuanze kutumia lugha ambayo tukikamilsha viongozi watatumia vizuri. Tukitumia lugha za Afrika zinatufanya tuwe watu zaidi kuliko kutumia lugha za kigeni.. Nafasi zipo ndani ya bara la Afrika hata nje ya bara la Afrika.  Mfano kwa Afrika Mashariki, Kiswahili kimetusaidia kutuunganisha na tutumie Kiswahili kwa ufasaha.

Stella Vuzo: Na sasa wito kwa wanaoadhimisha kimataifa

Mongella: Acheni kuiga mambo msiyoyajua! Watu wengi hawajui kiingereza vizuri, hawafahamu kifaransa vizuri wala kiarabu halafu mnang’ang’ania kuzungumza huku mnajiumauma. Kwa hiyo tumieni lugha ambayo mnaifahamu vizuri na mtajisikia vizuri kuwa ninyi ni watu wa bara la Afrika.