Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi na Kiswahili, hizi ni baadhi ya changamoto za kihistoria zilizotukwamisha - Dorothée Nshimimana

Picha ya maktaba, wanafunzi wakionesha nyaraka zao za kujiunga na Chuo Kikuu. Vyuo Vikuu vya Burundi kwa kiasi kikubwa hutumia lugha ya kifaransa na Kirundi.
UNHCR/A. Kirchhof
Picha ya maktaba, wanafunzi wakionesha nyaraka zao za kujiunga na Chuo Kikuu. Vyuo Vikuu vya Burundi kwa kiasi kikubwa hutumia lugha ya kifaransa na Kirundi.

Burundi na Kiswahili, hizi ni baadhi ya changamoto za kihistoria zilizotukwamisha - Dorothée Nshimimana

Utamaduni na Elimu

Lugha ya Kiswahili nchini Burundi inaendelea kushamiri hivi sasa ijapokuwa kwa kulinganisha na umri wake nchini humo, wanazuoni wanaona kuwa ukuaji wake umekuwa wa taratibu mno. 

Dorothée Nshimimana anayetambulika kuwa mwalimu wa kwanza kufundisha lugha ya Kiswahili katika vyuo vikuu nchini Burundi tangu mwaka 1993 aliporejea nchini humo baaada ya kuhitibu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika nchi jirani ya Tanzania, ni mmoja wa watu ambao kwa muda mrefu wamefanya utafiti kuhusu historia ya Kiswahili nchini Burundi.  

Bi Nshimimana alianzia kufundisha katika Chuo Kikuu cha Taifa Burundi, akaendelea katika vyuo vingine kikiwemo Chuo Kikuu cha Kijeshi Burundi, ISCAM. Mwalimu huyu ambaye pia ndiye mlezi wa vyama vyote vya Kiswahili nchini humo Burundi anaeleza changamoto za kihistoria zilizokizorotesha Kiswahili nchini humo. 

“Kiswahili hapa kwetu hakikuenea kama kilivyoenea katika nchi zingine, kwa nini…,” ndivyo anavyoanza Mwanazuoni Dorothée Nshimimana kuzitaja changamoto za kihistoria zilizokwamisha ukuaji wa lugha ya Kiswahili nchini mwake Burundi.  

Bi. Nshimimana anaitaja changamoto ya kwanza kuwa ni mbinu ya wakoloni ambao hawakuwapokea vizuri wafanyabiashara wa kiarabu na badala yake waliwatenga katika maeneo maalum ili Kiswahili kisienee.  

Anatoa mifano akisema waarabu walipofika maeneo mathalani Bujumbura, waliwekwa Buyenzi. Wakipita njia ya Kigoma, Tanzania, waishie Rumonge nchini Burundi na wasisambae katika maeneo mengine ya nchi. 

“Hata leo mkifanya utafiti, kila mkoa kuna sehemu ambayo inaitwa uswahilini kwa sababu ya ujanja wa wakoloni.” Anaeleza Bi. Nshimimana.  

Hata hivyo mwanazuoni huyo anaeleza kuwa lugha ni kama mafuriko makubwa ya maji, huwezi kuyazuia kwa mikono akitoa mfano kuwa kwa kuwa Kiswahili kilitumika kama lugha ya harakati za ukombozi, “kwenye redio za Afrika Mashariki sanasana kama Tanzania walikuwa wanaimba nyimbo za Kiswahili za kufukuza mkoloni. Wakati wanaimba hizo nyimbo zilikuwa zinakuja hata kwenye redio zetu za Burundi. Mwaka 1961 redio ya Burundi ilianza kutoa nyimbo za Kiswahili.” 

Changamoto ya pili anayoitaja Bi. NMsimimana, mwalimu huyu wa lugha ya Kiswahili kwa miaka mingi anasema ni wakati waarabu walipoingia nchini Burundi kupitia njia ya Ujiji, Kigoma Tanzania, wakipitia katika Ziwa Tanganyika na kabla ya kuingia ndani ya nchi ya Burundi wakaonwa na wenyeji ambao waliwashangaa na kwenda kutoa taarifa kwa Mfalme wa wakati huo kwamba kwa namna walivyoonekana waarabu hao ni kama walikuwa wanakuja kuivamia Burundi. Mfalme akatoa amri ya kupambana nao. Kutokana na mapigano kati ya wanamgambo wenyeji na waarabu waliojihami kwa bunduki, uhasama huo ukakwamisha kupokelewa kwa mikono miwili waarabu na maneno yao ya mchanganyiko wa kiarabu na kibantu na bila shaka ikawa kizuizi cha kiarabu kuchanganyika zaidi na kibantu cha wabantu wa Burundi. 

Hata hivyo kutokana na mapigano hayo ambapo waarabu walitumia maneno ya kiswahili ya ‘piga maliza wote’ ndimo lilimolzaliwa neno ‘Rumaliza’ lililonza kutumika nchini Burundi kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya rumaliza yaani lugha ya kuwamaliza warundi. 

Changamoto ya tatu, anaeleza Bi. Nshimimana kuwa ni namna waarabu walivyotumia maneno ya kiswahili kuwalazimisha wenyeji kuleta mali zao kwa wakoloni, mathalani wenyeji walipoambiwa, “leta mayai, leta siagia…leta..wakasema hii lugha ya kunyanganya warundi si lugha ya kusemwa. Tuiache.” 

Changamoto ya nne, ilikuwa ni namna wenyeji walivyokuwa wanapigwa viboko bila kujali rika wala hadhi yao katika jamii na kwa kawaida mtu akilazwa chini na kucharazwa viboko nane. Amri ilikuwa inasema ‘lalia nane’ yaani lala chini ili upigwe viboko nane. Hapo ndipo wenyeji yaani warundi wakaona hii lugha ya lalia nane, si lugha rafiki ya kusemwa.  

Changamoto ya tano, ilikuwa ni imani potofu iliyojengwa na warundi ambao ni wafugaji wa ng’ombe walipoamini kuwa mtu akizungumza lugha ya kiswahili, na mdomo huo huo ulioyatamka maneno ya kiswahili ukanywa maziwa ya ng’ombe, basi ng’ombe huo atakufa. Hata hivyo, miaka mingi baadaye, baada ya kiswahili kuwa kimejeruhiwa vibaya sana, mwanazuoni huyu Bi. Dorothée Nshimimana na wenzake walifanya utafiti na kuelimisha jamii kuwa suala hilo lilikuwa imani tu na halikuwa na ukweli wowote kwani hakukuwa na uhusiano kati ya uhai wa mifugo yao na lugha mpya ambayo wangeitumia. 

Hivi sasa Burundi ikiwa ni moja kati ya nchi 7 za Afrika Mashariki ambako Kiswahili kinazidi kushika kasi, wanajitahidi kuona ni kwa namna gani wanaweza kukifanya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zenye nguvu nchini humo ili waeze kuendana na eneo jingine la ukanda huo kwa ajili ya maeneo ya warundi wote.