Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano

Siku ya usaidizi wa kibinadamu twaelekea Bugambe, Uganda

Kila Agosti 19, dunia huadhimisha siku ya usaidizi wa kibinadamu ambapo mwaka huu maudhui ya siku hii ambayo lengo lake ni kuthamini mchango wa watu wanaotoa usaidizi wa kiutu pamoja na kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao wakati wa kutimiza wajibu huo ni utu wa pamoja. Tunaangazia kilichofanyika makao makuu ya umoja huo New York, Marekani na pia tutaungana na mwenzetu John Kibego aliyetembelea wakimbizi huko Uganda.

Mwanamuziki mwenye ulemavu wa kutoona anga’ra kimataifa

Kuwa mlemavu wa kutoona hakukumzuia kabisa mwanamuziki chipukizi kutoka Nigeria Cobhams Asuquo kushamiri hadi ngazi ya kimataifa.

Hii ni sehemu ya simulizi ya kusisimua katika makala iliyoandaliwa na Joseph Msami ambayo inaangazia juhudi za Shirika la Kimataifa la Haki Miliki WIPO kulinda na kuhifadhi haki za wabunifu, na wenye vipaji mbalimbali wakiwamo waimbaji.

Marimba ya Afrika yameota mizizi Colombia

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO linapigia chepuo utamaduni wa nyimbo kama sehemu ya kutunza urithi wa dunia katika mila na tamaduni mbali mbali. Muziki unaotumia ala za marimba ambao ni alama ya utamaduni wa watu wenye asili ya Afrika walioko maeneo mbali mbali duniani ikiwemo Ecuador na Colombia ni moja ya vitu ambavyo UNESCO inataka kuhifadhi. Joseph Msami katika makala ifuatayo anasimulia jinsi muziki huo unavyotumika kuhifadhi historia na hadhi ya watu hao wenye asili ya Afrika huko Colombia.

Nishati mbadala yabadilisha maisha ya jamii Uganda

Nchini Uganda wananchi wanatumia mbinu mbadala ya nishati kuendesha shughuli zao za kila siku na pia kupata kipato. Mbinu hizi ni moja ya juhudi za kupambana na umasikini na pia kulinda mazingira ikiwa ni baadhi ya malengo ya maendeleo endelevu.

Basi tuungane na John Kibego katika makala hii kufahamu zaidi.

Unyonyeshaji mtoto uanze saa moja tu baada ya mtoto kuzaliwa

Tarehe Mosi hadi Saba Agosti ya kila mwaka ni wiki ya Unyonyeshaji, siku ambayo Umoja wa Mataifa imetenga kuangazia jambo hili adhimu kwa makuzi ya mtoto na kwa mustakhbali wake wa baadaye. Shirika la afya duniani, WHO linasema kila mama mzazi anaweza kunyonyesha, alimradi apatiwe taarifa sahihi na jamii nayo imuunge mkono, sanjari na mfumo wa afya. Colostrum, ambayo ni maziwa yenye rangi ya manjano na mazito yatokayo pindi tu mama anapojifungua, yanaelezwa na WHO kuwa ni muhimu sana kwa mtoto aliyezaliwa na mama anapaswa kuanza kunyonyesha saa moja tu baada ya kujifungua.

Mwanamuziki kiziwi atumia muziki kupigania ujumuishwaji wa kijamii

Wakati mikutano ya mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha, IMF, mapema mwaka huu, palitokea mgeni mmoja aliyewashangaza wengi.

Signmark ni msanii wa muziki wa kufokafoka (au rap), kutoka Finland. lakini ajabu ilikuwa ni kwamba, yeye ni kiziwi. Wakati huo, alizungumzia jinsi alivyovunja sheria, kwa kuwa kiziwi wa kwanza kabisa kuwahi kupata mkataba wa kurekodi, na jinsi ambavyo amehamasisha umma kuhusu umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii.

Kufahamu zaidi, ungana na Joshua Mmali katika makala hii.

Joto kali lachangia ugumu wa maisha kambini

Maelfu ya wakimbizi kutoka Iraq wamesambaratishwa na vita, na wengi wao kuishia katika kambi mbali mbali zenye hali mbaya. Moja ya kambi hizo ni kambi iliyo ndani ya jangwa la Ameriyat al-Fallujah, huko nchini Iraq.

Katika makala hii tunakuletea madhila anayokumbana nayo mkimbizi mmoja na familia yake baada ya kufungasha virago kutokana na vita. Ungana na Joseph Msami kwa simulizi zaidi.

Ziara ya O’Brien Sudan Kusini yamulika mahitaji ya huduma na ulinzi

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, Stephen O’Brien yupo nchini Sudan Kusini kwa kwa ziara ya siku tatu ili kujionea na kutathmini hali ya kibinadamu, na kurejelea wito wa ufadhili.

Mpango wa kibinadamu nchini Sudan Kusini umetoa ombi la dola bilioni 1.3, lakini umepokea asilimia 40 ya fedha zinazohitajika.

Zaidi ya watu milioni moja na nusu ni wakimbizi wa ndani nchini Sudan Kusini, huku watu milioni 4.8 wakiwa hawana uhakika wa kupata chakula. Kumulika zaidi ziara ya Bwana O’Brien, ungana na Joshua Mmali katika makala hii.

Homa ya ini bado ni changamoto Uganda

Tarehe ishirini na nane Julai kila mwaka dunia huadhimisha siku ya homa ya ini. Shirika la afya ulimwenguni WHO huitumia siku hiyo kuhamasisha makabiliano dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, WHO inazitaka nchi wanachama kuchukua hatua haraka kuboresha ufahamu kuhusu homa ya ini, kuongeza fursa ya kufanyiwa vipimo na kupata huduma ya tiba.

Duniani kote watu milioni 40 wameambukizwa homa ya ini aina B na C, ikiwa ni mara 10 zaidi ya watu wanaoishi na VVU.

Tumenuia kutokomeza homa ya ini ifikapo 2030: Tanzania

Tarehe 28 mwezi Julai kila mwaka dunia inaadhimisha Siku ya Ugojwa wa Homa ya Ini. Ugonjwa huu unaongoza kwa maambukizi ukilinganishwa na virusi vya Ukimwi, lakini wengi hawautambui hata kuchukua hatua dhidi yake. Hii ni kauli ya shirika la afya ulimweguni WHO linalozihamasisha nchi wanachama kuchua hatua za tiba na elimu hima.

Kwa mujibu wa WHO watu milioni 40 Duniani kote wameambukizwa homa ya ini aina B na C, ikiwa ni mara 10 zaidi ya watu wanaoishi na VVU.