Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jarida la Habari

15 Februari 2021

Hii leo jaridani siku ya Jumatatu ni mada kwa kina na tunamulika nafasi ya redio katika jamii ya sasa na jinsi watangazaji walivyokwenda na wakati ili kuhakikisha chombo hicho adhimu kinaendelea kutekeleza majukumu yake. Katika kufanya hivyo tunakutana na Dina Marious wa kituo cha redio cha E-FM nchini Tanzania. Habari kwa ufupi tunamulika Ebola Guinea miongoni mwa taarifa muhimu. Mashinani tunaelekea nchini Kenya! Mwenyeji wako hii leo ni Grace Kaneiya, karibu!

Sauti
10'52"

12 Februari 2021

Hii leo jaridani ni mada kwa kina tunakwenda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kumulika kikosi kipya cha Tanzania, TANZBATT_8 katika kikosi cha kujibu mashambulizi (FIB) cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO. Tuna habari kwa ufupi ikimulika Tigray, Ethiopia na Yemen sambamba na mwaka mpya wa kichina unaoanza hii leo salamu ikiwa, Chun Jie Kuai Le! Kama kawaida ijumaa ni wakati wa kujifunza Kiswahili na tunakwenda Zanzibar hususan BAKIZA kufahamishwa maana ya maneno matano.

Sauti
10'22"

11 Februari 2021

Hii leo Jaridani Grace Kaneiya kutoka Nairobi Kenya anaanza Habari za UN akimmulika msichana kutoka Rwanda ambaye ni mhandisi wa magari kwenye kampuni ya magari ya Hyundai kwenye mji mkuu Kigali, ikiwa ni katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi. Kisha anakwenda Cameroon ambako radio imekuwa mkombozi kwa watoto ambao hawajakwenda shuleni kwa miaka mitatu sasa kutokana na mzozo nchini mwao. Sudan Kusini nako ukosefu wa amani wasababisha Umoja wa Mataifa kutoa wito kwa serikali kutekeleza haraka mkataba wa amani wa mwaka 2018.

Sauti
13'38"

10 Februari 2021

Jaridani hii leo Flora Nducha anaanza na taarifa ya changamoto kwa watengeneza chanjo dhidi ya COVID-19 duniani wakati huu ambapo chanjo za sasa zimeonekana kuwa dhaifu kwa mnyumbuliko mpya wa virusi vinavyosababisha Corona.  Anaangazia pia siku ya kimataifa ya mikunde hii leo ambapo taarifa inataja faida za mikunde kama vile maharagwe, kunde zenyewe, choroko na hata njugumawe. Nchini Uganda nako anabisha hodi kuona msaada wa UNICEF katika huduma za mama na mtoto na mashinani tunabisha hodi leo mashariki ya mbali, nchini Afghanistani.

Sauti
12'4"

09 Februari 2021

Jaridani hii leo Jumanne Februari 09 2021, Flora Nducha anaanzia Msumbiji kumulika msaada wa Umoja wa Mataifa kwa manusura wa kimbunga Eloise, wamejengewa makazi ya muda na huduma za kujisafi na maji safi. Kisha anakwenda Colombia ambako wakimbizi kutoka Venezuela wanazidi kumiminika wakikimbia madhila nchini mwao lakini taifa hilo mwenyeji linarasimisha uwepo wao. Taarifa nyingine ni kutoka Zimbabwe na shirika la FAO.

Sauti
13'29"

08 Februari 2021

Hii leo jaridani ni mada kwa kina ambapo Grace Kaneiya kutoka Nairobi Kenya anaangazia wanufaika wa mradi wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO nchini Tanzania katika kuwezesha wakulima mkoani Kigoma kulima maharagwe aina ya Jesca yenye virutubisho. N katika kuelekea siku ya kimataifa ya mikunde tarehe 10 mwezi Februari mwaka huu. Habari kwa ufupi tunaangazia India na maporomoko ya theluji, harakati za kukabili kuenea kwa Ebola iliyotangazwa kuibuka tena Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na mashinani anabisha hodi Lebanon akimulika pia harakati za FAO. Karibu!

Sauti
11'11"

05 Februari 2021

Leo Ijumaa ni mada kwa kina na Assumpta Massoi anakupeleka Nairobi Kenya ambako Grace Kaneiya katika kufuatilia utekelezaji wa mwaka wa kimataifa wa mboga mboga na matunda amevinjari kwa familia moja jijini Nairobi kuona mtazamo wao katika ulaji wa mboga za majani na matunda.

Sauti
10'39"

04 Februari 2021

Hii leo jaridani Grace  Kaneiya kutoka Nairobi nchini Kenya anaanzia na taarifa kuhusu siku ya saratani duniani ikimulika changamoto za upimaji wa gonjwa hilo wakati huu wa janga la COVID-19. Kisha anakwenda Morogoro nchini Tanzania kumulika tatizo la lishe duni na makuzi ya mtoto, halafu anakupeleka Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako amani imerejea katika mji wa Bangassou uliokuwa kitovu cha mashambulizi tarehe 3 mwezi uliopita.

Sauti
13'25"

03 Februari 2021

Leo Jumatano Flora Nducha anaanzia huko Madagascar ambako ukame wa muda mrefu umesababisha njaa kali na watu kulazimika kutengeneza rojo la ukwaju na kunywa huku wakilumangia na udongo mweupe. Kisha anakwenda Tigray nchini Ethiopia ambako nako hali si hali kwa wakimbizi wa ndani wakimbiao mapigano na wale waliotoka Eritrea. Hata hivyo WFP ambalo ni shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa  limetangaza mpango wake wa kusambaza kwa haraka chakula kwa wenye uhitaji zaidi barani Afrika.

Sauti
15'7"

02 Februari 2021

Hii leo jaridani Flora Nducha anaanza na ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu ikionesha kuwa wavulana wanaosafirishwa kiharamu idadi yao imeongezeka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Watu wengine wanasafirishwa pia kutumikishwa kwenye kuombaomba. Kisha atakufikisha Baidoa nchini Somalia kumulika hali ya kibinadamu na hatimaye Sudan Kusini ambako shule moja ya sekondari yaonesha uwezo wa wanafunzi wakimbizi.

Sauti
13'59"