Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Mtalaam wa UM apata hasira kuhusu mauaji ya mpalestina Hebron

Video ya raia wa Palestina aliyeuawa na askari wa Israel akiwa amejeruhiwa na kulala chini imemtia hasira mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya kiholela Christof Heyns.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kufuatia mauaji yaliyofanyika wili iliyopita mjini Hebron, kwenye ukingo wa magharibi, yakiripotiwa na shirika la haki za binadamu la Israel ambalo lilitoa video hiyo. Ripoti inaeleza kwamba mpalestina huyo amepigwa risasi baada ya kumchoma kisu askari wa Israel.

Ulinzi wa mambo ya kale ni suala la kimataifa:UNESCO

Ulinzi wa kazi za kihistoria za Sanaa sio tu suala la wakati wa migogoro au vita bali ni suala linalotia hofu kimataifa limesema shirika la Umoja wa mataifa la Elimu , Sayansi na Utamaduni UNESCO.

Huo pia ni mtazamo wa Dr Donna Yates mhadhiri wa usafirishaji haramu wa mambo ya kale na uhalifu wa Sanaa katika chuo kikuu cha Glasgow nchini Scotland.

Dr Yates anashiriki majadiliano kuhusu usafirishaji wa mali za kitamaduni yaliyoandaliwa na UNESCO mjini Paris leo Jumatano. Anaelezea ni maeneo gani hasa yaliyo katika hatari ya kuporwa.

(SAUTI YA DR YATES 1)

MONUSCO yaongezwa mwaka mmoja DRC

Baraza la Usalama leo limepitisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC MONUSCO kwa mwaka mmoja hadi Machi, 31, 2017, pia likiamua kutopunguza zaidi idadi ya walinda amani, hadi hali ya usalama itakapoimarika.

UN Photo/Iason Foounten

Kobler alaani mauaji ya raia Libya

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Martin Kobler, amelaani mauaji yaliyoripotiwa kufanyika Mashariki mwa Libya kwenye maeneo ya al-Tewibya na al-Zawiya.

Bwana Kobler amesema kwamba mauaji hayo ya raia ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu.

Taarifa iliyotolewa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL imeeleza kwamba vikundi vilivyojihami vimeripoti kuteka nyara wanaume kadhaa, kuwaua, pamoja na kuua na kujeruhi raia wengine wakiwemo watoto.

Maisha ya wakimbizi wa Mali nchini Burkina Faso hatarini

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuhudumia Wakimbizi UNHCR zimeonya kwamba maisha ya wakimbizi wa Mali 31,000 waliotafuta hifadhi nchini Burkina Faso yatakuwa hatarini iwapo hawataendelea kupewa msaada wa kibinadamu wa dharura.

Mkuu wa WFP nchini Burkina Faso ameeleza kwenye taarifa iliyotolewa leo kwamba wengi wa wakimbizi wanaoishi kambini wanategemea misaada ya kibinadamu tu kwa chakula na mahitaji yao ya msingi, akitegemea hali kuzorota zaidi wakati msimu wa mwambo ukikaribia.

Vijana wana jukumu kubwa katika vita dhidi ya ukimwi: Ndaba na Kweku Mandela

Wajukuu wa Hayati Nelson Mandela aliyekuwa Rais wa zamani wa Afrika Kusini na mwanaharakati wa kimataifa wa haki za binadamu, wamesema mchango wa vijana ni muhimu sana katika vita dhidi ya ukimwi.

Kweku Mandela na Ndaba Mandela wakizungumza kwenye kongamano la ukimwi mjini Moscow, Urusi wamesema wanaamini kazi wanayofanya ya kushiki kampeni ya vita dhidi ya ukimwi inasaidia hasa kuondokana na unyanyapaa na pia kuelimisha jamii kuona HIV na ukimwi ni kama maradhi mengine yanayohitaji mshikamano kuyakabili.

WHO yatangaza mwisho wa dharura ya Ebola kimataifa

Shirika la Afya Duniani (WHO), limetangaza leo kuwa mlipuko wa maambukizi ya virusi vya homa ya Ebola siyo tena suala la dharura linalotishia afya ya umma kimataifa, na kwamba hatari ya kuenea maambukizi ya Ebola kimataifa ni ndogo sana, kwani nchi sasa zina uwezo wa kukabiliana haraka na milipuko mipya.

Tangazo hilo limefuatia mkutano wa tisa wa Kamati ya Dharura ya WHO, kuhusu mlipuko wa homa ya Ebola Afrika Magharibi, ambao umefanyika kwa njia ya simu leo Machi 29, 2016 kuanzia saa sita na nusu hadi saa tisa na nusu za Geneva.

Mwandishi Florence Hartmann aachiliwa huru na mahakama ya kimataifa The Hague

Rais wa mfumo uliorithi mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa Rwanda na Yugoslavia ya zamani, MICT ametangaza leo kumwachilia mapema mwandishi wa habari Florence Hartmann.

Katika taarifa iliyotolewa na MICT, rais huyo ameeleza kwamba uamuzi huo umechukuliwa kutokana na tabia nzuri ya Bi Hartmann kwenye kifungo chake na kwa sababu tayari ametimiza zaidi ya theluthi mbili ya kifungo alichohukumiwa.