Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yaendesha kampeni dhidi ya Surua

Mtoto anapata chanjo dhidi ya Surua katika kampeni ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Beerta Muuri, Baidoa nchini Somalia. Picha: UM(Maktaba)

Somalia yaendesha kampeni dhidi ya Surua

Nchini Somalia, mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na serikali wamehitimisha kampeni ya siku tano ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Surua iliyolenga watoto milioni 4.2 nchini kote.

Watoto hao ni wale wenye umri wa kati ya miezi 6  hadi miaka 10 ambapo kampeni hiyo inafuatia visa zaidi ya elfu 23 vilivyoripotiwa mwaka jana, idadi ambayo ni kubwa kulinganisha na miaka iliyotangulia.

Mwakilishi wa shirika la afya ulimwenguni, WHO nchini Somalia, Ghulam Popal amesema ni kipaumbele cha shirika lake kuendelea kusaidia serikali ili kudhibiti mlipuko wa surua.

image
Kinamama na watoto wapanga foleni kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Beerta Muuri Baidoa nchini Somalia. Kampeni hiyo imewezeshwa na UNICEF. Picha: UM (Maktaba)
Kwa mantiki hiyo amesema WHO pamoja na shirika la kuhudumia watoto duniani, UNICEF waliungana na serikali kuhakikisha chanjo inatolewa kwa kiwango kikubwa.

Naye mwakilishi wa UNICEF Somalia, Jesper Moller amesema pamoja na mafanikio ya utoaji wa chanjo hiyo, bado kuna tishio akisema njia pekee ya kulinda watoto ni kuendesha kampeni za aina hiyo.

Amesema kampeni watakayofanya mwaka huu dhidi ya Surua itaenda sambamba na utoaji w amatone ya Vitamin A kwa watoto.