Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo mpya dhidi ya homa ya matumbo yapitishwa

Daktari UNRWA anachunguza mtoto huko Yalda, Damascus, Syria, katika harakati za kudhibiti ugonjwa wa homa ya maumbo. Picha: UNRWA

Chanjo mpya dhidi ya homa ya matumbo yapitishwa

Chanjo yenye uthabiti zaidi dhidi ya ugonjwa wa homa ya matumbo au kuhara damu imepitishwa na shirika la afya ulimwenguni, WHO. Taarifa zaidi na John Kibego.

(Taarifa ya John Kibego)

Ikiwa na jina la TCV, chanjo hiyo ni bunifu, na pamoja na kutoa kinga ya muda mrefu kuliko chanjo za sasa, mtumiaji anahitaji dozi chache.

WHO inasema zaidi ya hayo, chanjo hiyo inaweza kupatiwa watoto wenye umri wa kuanzia miezi 6 kupitia mpango wa utoaji wa chanjo kwa watoto.

Kitendo cha WHO kutangaza kuwa chanjo hiyo TCV inakidhi vigezo, kina maana kwamba sasa inaweza kununuliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la watoto, UNICEF na ushirika wa chanjo duniani, GAVI na kusambazwa kwenye nchi za kipato cha chini ambako homa ya matumbo au Typhoid imekuwa na madhara makubwa.

Ni katika nchi hizo ambako ambako mara nyingi watoto au watu wazima hupatiwa viuavijasumu au antibayotiki kwa homa tu inayodhaniwa kuwa ni homa ya tumbo na hatimaye kusababisha usugu wa dawa.

Tayari GAVI imepitisha dola milioni 85 kwa ajili ya ununuzi wa chanjo hiyo ya TCV kuanzia mwaka ujao wa 2019.

Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka homa ya matumbo husababisha vifo vya zaidi ya watu laki moja na elfu sitini, idadi ambayo ni kati ya wagonjwa milioni 11 hadi milioni 20.

Kwa mujibu wa WHO ukuaji wa miji, mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa mipango miji bora ni miongoni mwa sababu za kuenea kwa homa ya matumbo.