Mapigano yasitishwa mji mkuu Sana’a na sasa yahamia viungani

5 Disemba 2017

Nchini Yemen baada ya mfululizo wa mashambulizi ya anga na ardhini kuanzia mwishoni mwa wiki kwenye mji mkuu Sana’a, hatimaye hii leo mashambulizi yamekoma na hivyo wananchi kuweza kuibuka kutoka kwenye makazi yao ili kupata huduma.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mjini humo, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Jamie McGoldrick amesema siku tano za machungu zimekoma baada ya kusabaisha vifo vya watu wapatao 125 na mamia ya majeruhi.

Hata hivyo amesema bado wana taarifa za baadhi ya watu kusalia wamenasa kwenye majumba yao kutokana na hofu, akitaja miongoni mwao kuwa ni wanawake wajawazito pamoja na majeruhi.

Amesema kwa sasa mapigano yamehamia kwenye viunga vya mji wa Sana’a ambako vikosi vya kimataifa vinavyomuunga Rais Abd Mansur Hadi vinakabiliana na waasi wa kihouthi.

Halikadhalika Bwana McGoldrick amesema tayari timu kutoka Umoja wa Mataifa imeelekea Saudi Arabia katika jaribio la kusaka kulegezwa kwa vizuizi vya misafara nchini Yemen.

Moja ya malengo ya msafara huo ni kulegeza vikwazo kwenye bandari ya magharibi ya Hodeida ili kuweza kuruhusu meli kupakua shehena muhimu zinazohitaka ikiwemo petrol, dizeli, mafuta ya kula, chakula na dawa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter