Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Mshauri mpya wa Kijeshi kwa DPKO amewasili Makao Makuu kuanza kazi

Liuteni Jenerali Chikadiba Obiakor wa Nigeria, Mshauri wa Masuala ya Kijeshi katika Idara ya UM Kuhusu Operesheni za Ulinzi wa Amani (DPKO) amewasili New York Alkhamisi kuanza kazi. Jenerali Obiakor amedhaminiwa madaraka ya kuishauri Idara ya DPKO juu ya masuala yote ya kijeshi yanayofungamana na shughuli za ulinzi amani za UM.

Wakulima wanahimizwa kujiunga na mapinduzi ya "Kijanikibichi"/Kilimo

Wajumbe karibu 100 kutoka nchi 36 wanaokutana kwenye Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo (FAO)Roma, Utaliana wiki hii wametoa mwito maalumu wenye kupendekeza kwa wakulima wa kimataifa kujihusisha na yale mapinduzi ya kilimo yanayoendelea, yajulikanayo kama mapinduzi ya "Kijanikibichi". Mapinduzi haya huwakilishwa na utaratibu unaojulikana kama "Mfumo wa Hifadhi Bora ya Ukulima" au Mfumo wa CA.

FAO yanasihi kilimo cha mihogo kiimarishwe kujikinga njaa kwa nchi masikini

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeripoti matukio ya utafiti yaliothibitisha kihakika kwamba zao la nchi za joto la mhogo lina uwezo mkubwa wa kuzisaidia nchi masikini kupata chakula na nishati kwa usalama wa kudumu, hasa yale mataifa yenye kuhatarishwa na athari za kupanda kwa kasi kwa bei za chakula na mafuta katika soko la kimataifa.

OCHA imeripoti Wakongo 65,000 wafukuzwa Angola

Christophe Illemassene, Msemaji wa Shirika la UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) katika JKK ameiambia Redio ya UM-Geneva kwamba wana taarifa iliothibitisha kuwa tangu Mei mwaka huu raia wa Kongo 65,000 walifukuzwa na kuondoshwa kutoka Angola, wingi wao wakiwa wale wahamiaji walioingia Angola bila sheria, wakitafuta ajira kwenye viwanda vya migodi.

Tume ya waliotoweka bila khiari duniani inakutana Argentina

Tume ya Utendaji ya UM juu ya Watu Waliolazimishwa Kutoweka na Kupotea Bila Khiari inakutana katika mji wa Buenos Aires, Argentina kuanzia Julai 24 mpaka 26 kufanya mapitio ya kesi za watu 300 waliotoweka duniani, kuambatana na matatizo ya kisiasa. Tume hiyo ina wajumbe wataalamu watano na inakutana, kwa mara ya kwanza katika taifa la Amerika ya Latina la Argentina, taifa ambalo katika miaka ya sabini na mwanzo wa miaka ya themanini liliathirika sana na tatizo la kupotea kwa wapinzani wingi wa kisiasa, bila ya aila zao kujua walipo.

Mawaziri wa Maziwa Makuu wamekusanyika Kinshasa kuzingatia taasisi ya haki za wanawake

Mawaziri wanaohusika na haki za wanawake kutoka mataifa 11 ya Maziwa Makuu katika Afrika wameanza, Alkhamisi (24/07/08) mijadala ya siku mbili kwenye mji wa Kinshasa, katika Jamhuti ta Kideomkrasi ya Kongo (JKK) kuzingatia hatua za kuchukuliwa kipamoja kuanzisha taasisi mpya ya kikanda itakayoendeleza utafiti juu ya haki za kijinsiya na kushughulikia huduma za kuhifadhi nyaraka zinazoambatana na kadhia hiyo.

Kwa Ufupi:

Baada ya kushauriana na Raisi wa Baraza Kuu, pamoja na Wenyekiti wanaowakilisha makundi matano ya kikanda yanayohusiana na Mataifa Wanachama, KM wa UM ameripoti kwa Baraza Kuu uamuzi wake wa kumteua Navanethem Pillay wa Afrika Kusini kuwa Kamishna Mkuu mpya wa UM juu ya Haki za Binadamu baada ya Jaji Louise Arbour wa Kanada, ambaye alimaliza muda wa kazi, baada ya iaka mitano na UM, mnamo Juni 30 2008. Tangu 2003 Pillay alikuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Halaiki (ICC) na kabla ya hapo, katika 1999 aliteuliwa kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR), taasisi ambayo alijiunga nayo 1995 baada ya kuteuliwa na Baraza Kuu; na mnamo 1998 Jaji Pillay aliongezewa muda wa kutumikia Mahakama ya ICTR kwa miaka minne zaidi.

ECOSOC inazingatia uhusiano bora na mataifa yanayofufuka migogoro

Baraza la Uchumi na Maendeleo la UM (ECOSOC), linalokutana Makao Makuu kwa sasa, linaeendelea na mijadala ya kuzingatia masuala maalumu ya kuimarisha uhusiano bora, na wa kuridhisha, na zile nchi zinazojitahidi kuibuka kutokana na athari na mabaki ya migogoro. ECOSOC pia inasialia taratizu za kupanua ushirikiano wake na ile Kamisheni ya UM juu ya Ujenziamani, kwa makusudio ya kuendeleza zaidi juhudi za muda mrefu za kufufua shughuli za kiuchumi na jamii kwenye maeneo husika.

Ndege zilizobeba madawa ya kulevya zimekamatwa Guinea-Bissau

Kwenye taarifa iliotolewa na Shola Omoregie, Mjumbe wa KM kwa Guinea-Bissau iliripoti kushikwa kwa ndege mbili na watu wa usalama nchini Guinea-Bissau, ndege ambazo zinatiliwa shaka zimebeba shehena ya madawa ya kulevya. Kwa mujibu wa ripoti, baadhi ya watu wanaohusika na ndege hizo wamewekwa kizuizini kwa sasa wakisubiri matokeo ya uchunguzi juu ya fungamano walionayo na biashara ya madawa ya kulevya.

Mjumbe wa KM kwa Usomali ajasirisha BU kudumisha amani haraka katika Pembe ya Afrika

Ahmedou Ould-Abdallah, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali leo asubuhi alipohutubia mbele ya Baraza la Usalama juu ya hali katika Usomali aliwakumbusha wajumbe wa Baraza kuhusu wajibu walionao wa kuzingatia, kwa ujasiri mkubwa, uwezekano wa kubadili hadhi ya vikosi vya ulinzi wa amani vya UA vya AMISOM viliopo Usomali, ili vikosi hivyo vidhaminiwe madaraka mapya na viwe vikosi vya amani vya UM.