Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa Ufupi:

Kwa Ufupi:

Baada ya kushauriana na Raisi wa Baraza Kuu, pamoja na Wenyekiti wanaowakilisha makundi matano ya kikanda yanayohusiana na Mataifa Wanachama, KM wa UM ameripoti kwa Baraza Kuu uamuzi wake wa kumteua Navanethem Pillay wa Afrika Kusini kuwa Kamishna Mkuu mpya wa UM juu ya Haki za Binadamu baada ya Jaji Louise Arbour wa Kanada, ambaye alimaliza muda wa kazi, baada ya iaka mitano na UM, mnamo Juni 30 2008. Tangu 2003 Pillay alikuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Halaiki (ICC) na kabla ya hapo, katika 1999 aliteuliwa kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR), taasisi ambayo alijiunga nayo 1995 baada ya kuteuliwa na Baraza Kuu; na mnamo 1998 Jaji Pillay aliongezewa muda wa kutumikia Mahakama ya ICTR kwa miaka minne zaidi.

Shirika la Muungano wa UM/UA Kulinda Amani Darfur (UNAMID) limeripoti kuwasili Darfur, kutokea Cairo, kundi la mwanzo la vikosi vya Wahandisi wa Misri 126 wanaotarajiwa kushirikiana na wanajeshi 83 wenziwao waliotangulia na walioenezwa katika mji wa El Fasher. Baadhi ya wanajeshi hawo wa Misri sasa wanashiriki katika ujenzi wa kiwanja cha ndege cha El Fasher, ambacho kitakapomalizika kinatarajiwa kurahisisha shughuli na operesheni za UNAMID kwa ujumla katika Sudan Magharibi.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamekutana Alkhamisi asubuhi, kwenye kikao cha faragha, kufanya makadirio ya kazi za ulinzi amani za UM katika Cote d'Ivoire. Yong-jin Choi, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire alilipatia Baraza tathmini kamili ya hali halisi ya usalama na amani nchini humo. Alasiri Baraza la Usalama limepanga kushauriana juu ya Myanmar, ambapo Mshauri Maalumu wa KM kwa Myanmar, Ibrahim Gambari atahudhuria. Kadhalika, Ijumatano (24/07/08) jioni Naibu KM Anayehusika na Operesheni za Amani za UM, Jean-Marie Guehenno aliwakilisha mbele ya Baraza la Usalama ripoti mpya kuhusu maendeleo kwenye kazi za UM za kuimarisha usalama na amani zinazosimamiwa na MONUC katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Gholam-Reza Aghazadeh, Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran ametarajiwa kukutana Alkhamisi mjini Vienna, Austria na Mohamed ElBaradei, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) kuzingatia ushirikiano katika udhibiti bora wa miradi ya nishati za nyuklia katika Iran.

Shirika la UM juu ya Huduma za Kufarajia Wahamiaji wa Kifalastina (UNRWA) limeripoti kwamba hali ya ufukara katika Tarafa ya Ghaza inazidi kuharibika, ambapo imegunduliwa zaidi ya nusu za kaya zote katika eneo hilo zinaishi maisha ya kiwango cha chini ya kiwango rasmi cha umasikini, ambapo asilimia 51.8 ya kaya zinategemea misaada ya kiutu, na ambapo ukosefu wa kazi unakaribia asilimia 30, hususan miongoni mwa vijana wa Kifalastina.