Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Operesheni za amani Ethiopia/Eritrea zaongezewa muda na Baraza la Usalama

Baraza la Usalama, kwa kauli moja, limepitisha azimio la kuongeza muda wa operesheni za amani mipakani Ethiopia na Eritrea kwa miezi sita zaidi, kwa sababu imeripotiwa hali ya wasiwasi bado inaendelea kukithiri kwenye lile eneo la kusitishwa mapigano la TSZ. Mataifa haya mawili vile vile yalinasihiwa kuondosha haraka vikosi vyao ambavyo hivi sasa vimeenezwa kwenye eneo la mgogoro la TSZ.

KM azuru makumbusho ya Mauaji ya Halaiki Rwanda

KM Ban alikuwepo Kigali, Rwanda mwanzo wa wiki na alizuru Makumbusho ya Mauaji Makubwa ya Halaiki. Alisema alihuzunishwa sana na aliyoyashuhudia, na alitoa mchango binafsi wa dola 10,000 kufadhilia mfuko wa Serikali ambao hutumiwa kuwasaidia mamia ya watoto mayatima wa mauaji hayo kupata elimu.

Watoto wadogo bado wanaendelea kuajiriwa kupigana

Ripoti mpya ya KM juu ya hali ya watoto katika maeneo yenye mapigano imebainisha kwamba kuna baadhi ya nchi wanachama ambazo bado zinaendeleza karaha ya kuwalazimisha watoto wadogo kujiunga na makundi ya wanamgambo na kushiriki kwenye mapigano. Mataifa haya, kwa mujibu wa ripoti ya UM, hujumuisha Afghanistan, Burundi, Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Colombia na vile vile Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Myanmar, Nepal, Philippines, Somalia, Sudan pamoja na Sri Lanka na Uganda.