Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA

LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA
Lugha ya kiswahili kuadhimishwa kimataifa kila tarehe 7 Julai - UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO tarehe 23 mwezi Novemba mwaka 2021 lilitangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu ni Kiswahili kwa amani na ustawi. Lengo hasa la maadhimisho haya ya mwaka ni kusongesha matumizi ya lugha ya kiswahili kama nguzo ya amani, na ustawi na wakati huo kuimarisha tamaduni mbalimbali.

UNESCO ilipitisha uamuzi huo huko makao makuu yake mjini Paris Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo.
Azimio lilipitishwa bila kupingwa na utekelezaji wake unaanza mwaka huu wa 2022.

Kupitia ukurasa huu mahsusi, utapataa taarifa zote kuanzia kupitishwa kwa azimio hilo, mapokeo yake na harakati za kukuza lugha ya Kiswahili ili iweze kujenga amani, uchumi, maendeleo na utangamano katika kona mbali mbali za dunia.

Utapata taarifa zilizochapishwa, video kutoka watu mbalimbali iwe maafisa wa serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, maafisa wa UN wenyewe, wanazuoni, wanafunzi na wananchi wa kawaida.


 

Tuondoe vikwazo vya kitamaduni na kimazingira dhidi ya watu wenye ulemavu- Guterres

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu, Umoja wa Mataifa unapigia chepuo marekebisho yatakayoondoa vikwazo dhidi ya kundi hilo ili malengo ya maendeleo endelevu yanufaishe watu wote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake amesema msingi mkuu wa kufanikisha hilo ni kuweka mazingira ambamo kwayo hakuna mtu atakayeona ametengwa au ameenguliwa katika kufanikisha malengo hayo.

Mathalani amesema kuwepo kwa miundombinu, teknolojia, huduma na bidhaa ambazo zitanufaisha watu wote wakiwemo watu bilioni moja wenye ulemavu duniani.

Utumwa wa kisasa wazidi kuleta mateso- UM

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza utumwa ambapo Umoja wa Mataifa unasema kuwa hivi sasa zaidi ya watu milioni 40 duniani kote ni waathirika wa utumwa.

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kazi duniani, ILO unasema ijapokuwa utumwa wa kisasa bado haujatambulika kisheria, kitendo hicho kinatumika kuficha madhila mengi.

Madhila hayo ni pamoja na utumikishaji, kuweka watu rehani kwa madeni, ndoa za lazima na usafirishaji haramu.

Kama hiyo haitoshi, zaidi ya watoto milioni 150 wanatumikishwa, na hii ikimaanisha ni takribani mtoto mmoja katika kila watoto 10.

Picha na UM

Wasaka hifadhi na wakimbizi vijana waona nuru huko Ujerumani

Stahamala na utangamano ni mambo ambayo Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake ikiwemo lile la wakimbizi duniani, UNHCR unapigia chepuo kila uchao. Hatua hiyo inatatokana na ukweli kwamba mambo hayo mawili ni muhimu wakati huu ambapo idadi ya watu wanaosaka hifadhi ugenini inaongezeka kila uchao. Stahamala huwezesha watu wa rangi,  jinsia au utaifa tofauti kuishi pamoja na hivyo kuimarisha ustawi wao. Na hivyo ndiyo inavyofanyika huko Ujerumani, nchi ambayo inapokea wakimbizi na wahamiaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita. Je nini kinafanyika?