Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumwa wa kisasa wazidi kuleta mateso- UM

Utumwa wa kisasa wazidi kuleta mateso- UM

Pakua

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza utumwa ambapo Umoja wa Mataifa unasema kuwa hivi sasa zaidi ya watu milioni 40 duniani kote ni waathirika wa utumwa.

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kazi duniani, ILO unasema ijapokuwa utumwa wa kisasa bado haujatambulika kisheria, kitendo hicho kinatumika kuficha madhila mengi.

Madhila hayo ni pamoja na utumikishaji, kuweka watu rehani kwa madeni, ndoa za lazima na usafirishaji haramu.

Kama hiyo haitoshi, zaidi ya watoto milioni 150 wanatumikishwa, na hii ikimaanisha ni takribani mtoto mmoja katika kila watoto 10.

Wanawake na watoto wa kike nao ni waathirika zaidi ambapo ni asilimia 99 ya watumikishwaji kwenye ukahaba.

Kwa kuzingatia hilo, ILO imeridhia nyaraka mpya yenye nguvu kisheria ambayo unalenga kuimarisha jitihada za kimataifa za kutokomeza utumikishaji watu.

Nyaraka hiyo ilianza kutekelezwa mwezi Novemba mwaka 2016 na tayari kuna kampeni ya kushawishi nchi angalau 50 ziridhie ili iweze kuanza kutumika rasmi ifikapo mwakani.

Photo Credit
Sanaa ikitumika kuonyesha madhila ya utumwa. Hapa ni kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika moja ya matukio ya kukumbuka siku ya kutokomeza utumwa. (Picha:: UN /Devra Berkowitz)