Tuondoe vikwazo vya kitamaduni na kimazingira dhidi ya watu wenye ulemavu- Guterres
Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu, Umoja wa Mataifa unapigia chepuo marekebisho yatakayoondoa vikwazo dhidi ya kundi hilo ili malengo ya maendeleo endelevu yanufaishe watu wote.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake amesema msingi mkuu wa kufanikisha hilo ni kuweka mazingira ambamo kwayo hakuna mtu atakayeona ametengwa au ameenguliwa katika kufanikisha malengo hayo.
Mathalani amesema kuwepo kwa miundombinu, teknolojia, huduma na bidhaa ambazo zitanufaisha watu wote wakiwemo watu bilioni moja wenye ulemavu duniani.
Kwa mantiki hiyo Bwana Guterres ametaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutumia siku ya leo ya watu wenye ulemavu duniani kuondoa vikwazo vya kimazingira na kiutamaduni na hivyo kujenga jamii ambazo zinaweza kukabiliana na mazingira yake na pia kuweka fursa za kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.