Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Demokrasia duniani iko njia panda- Ripoti

Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa ripoti ya kwanza kuhusu hali ya demokrasia ulimwenguni huko Geneva, Uswisi. Picha: UM/Video capture

Demokrasia duniani iko njia panda- Ripoti

Demokrasia duniani iko njia panda na hatua lazima zichukuliwe ili kuilinda na kuiheshimu, imesema ripoti ya kwanza iliyozinduliwa leo huko Geneva, Uswisi kuhusu hali ya demokrasia ulimwenguni.

Ripoti hiyo pamoja na kutambua kuendelea kuchipua kwa demokrasia duniani, pia imeweka bayana kusuasua kwa maendeleo ya demokrasia katika muongo uliopita huku changamoto na vitisho dhidi ya demokrasia vikibainika katika baadhi ya nchi na maeneo.

Mathalani ripoti inaonyesha jinsi serikali zinavyoendelea kukabiliwa na changamoto za kufuatiliwa na mabunge, mahakama na vyombo vya habari kama njia mojawapo za kuziwajibisha.

Na kwa upande mwingine demokrasia inakwama kutokana na rushwa, siasa za pesa, ukosefu wa usawa na baadhi ya jamii kutengwa.

Akizindua ripoti hiyo, Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amesema ingawa kasi ya kukua kwa demokrasia ni ndogo lakini ikilinganishwa na mwaka 1975 kuna maendeleo.

Amesema wakati huo ni theluthi moja tu ya nchi zilionekana kuwa na demokrasia lakini hivi sasa ni theluthi mbili ya nchi ambazo zimehusika katika utafiti huo ambao unachambua hali ya kidemokrasia duniani.

Hivyo amesema..

(Sauti ya Kofi Annan)

“Demokrasia ni itikadi muhimu zaidi ambayo serikali ulimwenguni zimewahi kushuhudia.”

Kwa mantiki hiyo Bwana Annan amesema..

(Sauti ya Kofi Annan)

“Matokeo na ujumbe wa ripoti hii siyo tu yanafaa kwa marejeo ya wasomi, bali ni mchango wa msingi kwenye uwezeshaji wananchi katika ustawi wa demokrasia.”

Ripoti hiyo imeandaliwa na taasisi ya kimataifa kaw ajili ya demokrasia ya usaidizi wa uchaguzi, IDEA.