Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa maji kuendelea kuchochea ukosefu wa usalama duniani- Guterres

Uhaba wa maji nchini Sudan Kusini siyo tu ni tishio kwa amani na usalama bali pia maendeleo kwa kuwa wananchi wanatumia maji yasiyo safi na salama na kupata magonjwa. (Picha:Unifeed video)

Uhaba wa maji kuendelea kuchochea ukosefu wa usalama duniani- Guterres

Vitisho vya amani,  usalama na utulivu duniani vinaongezeka na kuimarika kila uchao na hivyo kusababisha mazingira magumu zaidi ya kutatua mizozo duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana leo kujadili jinsi ya kushughulikia changamoto za kisasa za amani na usalama duniani.

Ametolea mfano uhaba wa maji akisema yakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 mahitaji ya maji duniani yataongezeka kwa asilimia 40 na hivyo kuibua mzozo baina ya watu.

Maendeleo ya teknolojia nayo amesema licha ya kuleta mafanikio makubwa pia yamerahisisha mawasiliano baina ya vikundi vya kigaidi na hata utumikishaji wa watu kwenye vikundi hivyo hivyo akasema..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Hebu na tufanye kazi pamoja ili tuimarishe harakati za Baraza hili za kushughulikia mambo mapya yanayoibuka na kupanua mifumo ya kufanyia kazi, kuongeza rasilimali za kuzuia mizozo na pia kuwa na mfumo thabiti wa kuepusha mizozo na kuendeleza amani.”

image
Maendeleo katika mitandao yameleta faida kubwa lakini pia hasara kwa kuwa sasa watu wasio na nia njema wanatumia mitandao kutumikisha watu kwenye vikundi vya misimamo mikali. Nchi sasa zimechukua hatua kuweka usalama kwenye mitandao. (Picha:ITU)
Na zaidi ya yote Katibu Mkuu akasema..

“Hebu nisisitize umuhimu wa umoja ndani  ya Baraza la Usalama. Bila umoja, pande kinzani kwenye mizozo zinaweza kuchukua misimamo ambamo kwayo sasa vichocheo vya mizozo vitafanya hali kuwa mbaya zaidi tena na tena. Lakini kuwa na umoja, tunaweza kusongesha usalama na ustawi wa wote.”