Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali wekeza dola 1 katika afya upate dola 20 za mapato- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kushoto) huko Tokyo, Japan akihutubia jukwaa la afya kwa wote. Picha: UM

Serikali wekeza dola 1 katika afya upate dola 20 za mapato- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres yuko Tokyo nchini Japan ambako amekuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hizo Shinzo Abe.

Katika mkutano wao na waandishi wa habari, Bwana Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya usalama kwenye rasi ya Korea.

Amesema kila mtu anataka kuepusha hali isiwe mbaya zaidi na kwamba nia mbaya zinachochea nchi kujiingiza kwenye mazingira yanayoweza kutumbukiza dunia kwenye vita, hali ambayo amesema itakuwa na madhara makubwa.

Bwana Guterres amerejelea kuwa maazimi ya Baraza la Usalama kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini ni lazima yatekelezwe kwa kina.

Akiwa Tokyo Bwana Guterres pia amezungumza kwenye jukwaa kuhusu afya kwa wote duniani ambako amesema kila dola moja inayowekezwa katika sekta ya afya inazalisha dola 20 katika ukuaji wa uchumi.

Amesema uwekezaji huo unasaidia kila mtu kupata huduma za afya popote pale alipo na kwa wakati anaotaka na hivyo kuepusha pengo linalotokea katika utoaji wa huduma za afya.

Ametoa mfano wa ugonjwa wa Kifua Kikuu akisema mwaka jana pekee zaidi ya visa vipya milioni 4.1 havikuweza kuripotiwa kutokana na ukosefu wa vituo vya uchunguzi.

image
Harakati za kutokomeza kipindupindu Somalia na kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa watoto. Picha: WHO
(Sauti ya Antonio Guterres)

“Upatikanaji wa huduma ya afya kwa wote ni sawa na mwamvuli muhimu wa kuzuia pengo hilo. Kupitia mifumo thabiti ya afya inayoendana an mazingira ya watu na haki za binadamu, huduma za afya zinaweza kuwa bora na hata fursa za kuzifikia zinaboreshwa.”

Hata hivyo amesema..

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kulia) huko Tokyo, Japan akihutubia jukwaa la afya kwa wote. Picha: UM
(Sauti ya Antonio Guterres)

“Utashi wa kisiasa ni muhimu katika kufungua uwekezaji huu. Na hakuna mpango mmoja kwa wote ni lazima kila nchi ijipangie njia yake kuelekea huduma ya afya kwa wote. Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia uendelezaji na utekelezaji wa mipango ya kitaifa ya kunufaisha watu wote.”