Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Mdogo juu ya Masuala ya Kiutu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, John Holmes, Ijumaa alikamilisha ziara ya siku mbili katika mji wa Juba, Sudan Kusini ambapo alikutana, kwa mazungumzo na wawakilishi wa serikali ya jimbo. Aliwaahidi UM utawasaidia kukabiliana na masuala muhimu ya kijamii, hususan yale yanayofungamana na sekta ya afya. Kabla ya hapo, Holmes alikutana na Raisi wa Sudan kusini, Salva Kiir na walishauriana taratibu zinazohitajika kuharakisha utekelezaji kamili wa mapatano ya jumla ya amani katika eneo la Sudan kusini.

Kuhusu hali katika Kivu Kaskazini, Shirika la Ulinzi Amani la UM katika JKK (MONUC) limeripoti mapambano kutukia kwenye eneo hili, baina ya makundi ya waasi, wafuasi wa Jenerali Mtoro Laurent Nkunda na jeshi la mgambo la PARECO. Hakujapokelewa taarifa hakika zenye kuelezea kama kuna wapiganaji waliojeruhiwa. Kadhalika MONUC imeripoti mapigano yalifumka kati ya waasi wafuasi wa Nkunda na wapiganaji wa kikabila wa Mai-Mai, katika zile sehemu za miji karibu na mipaka na Uganda, hali iliosababisha raia kung’olewa makazi. Sehemu za kaskazini, katika eneo la Kivu Kaskazini hali huko ni ya kuridhisha kidogo, ambapo mashirika ya kimataifa yanayohudumia misaada ya kihali yameweza kuendeleza shughuli zao na ambayo, hata iliruhusu baadhi ya wahamiaji wa ndani kurejea vijijini mwao.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeeleza mapigano ya karibuni kwenye mji wa Mogadishu, Usomali yalisababisha raia 55 kuuawa, ikijumlisha watoto sita. Vurugu hili limesababisha tena watu, na aila zao, kuhajiri Mogadishu na kuelekea kwenye kambi za wahamiaji wa ndani, katika barabara ya Afgooye-Mogadishu, palipoanzishwa makazi ya muda kwa watu 360,000. OCHA inasema watu 100,000 walishahama makwao, tangu Septemba, kukimbia vurugu. Idadi ya watu waliong’olewa makazi, mwaka huu pekee, kutoka mji mkuu wa Mogadishu, inakadiriwa kufikia watu 250,000. Wakati huo huo, manowari za nchi wanachama wa Umoja wa NATO, na zile za Uholanzi, zilifanikiwa kuongoza meli tatu za Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) kukamilisha safari, na kuzikinga na maharamia wanaotangatanga kwenye mwambao wa Usomali. Meli zilikuwa zimechukua tani 18,730 za chakula kuhudumia umma muhitaji wa Usomali.

Wajumbe wa kutoka Mataifa Wanachama wa UM wamekusanyika wiki hii kwenye mji wa Doha, Qatar kuhudhuria mkutano wa siku nne, kufuatilia utekelezaji wa Makubaliano ya 2002 ya Monterrey, Mexico, ya kufadhilia fedha za kukuza uchumi na maendeleo ya jamii katika nchi zinazoendelea. Muafaka huu baina ya nchi za Kaskazini na Kusini ya dunia ulikuwa ni wa kihistoria. Kwenye mkesha wa mkutano, leo Ijumaa, KM Ban Ki-moon na Emir wa Qatar walifanyisha majadiliano, yasio rasmi, ya hadhi ya juu kusailia athari za mgogoro wa fedha, uliojiri karibuni katika soko la kimataifa, kuhusu huduma za maendeleo, na katika udhibiti wa mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na juhudi za kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi kuendeleza kadhia zamaendeleo. Majadiliano haya ya faragha, yalifanyika siku moja kabla ya Mkutano Mkuu wa Kufadhilia Fedha za Kukuza Maendeleo kuanza mijadala yake, na yalihudhuriwa wajumbe wa kimataifa 30, ikijumlisha viongozi 10 wa mataifa, serikali na mashirika ya kimataifa. Tutakupatieni ripoti za mkutano baadaye.