Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Baraza la Usalama linazingatia Chad na JAK

Baraza la Usalama Ijumaa limezingatia ripoti ya karibuni ya KM juu ya hali ya usalama katika Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK). Ndani ya ripoti KM amependekeza UM upeleke vikosi vya kulinda amani vya UM vya wanajeshi 6,000 wanaotakikana kuchukua nafasi ya vikosi vya Umoja wa Ulaya viliopo Chad mashariki na kaskazini-mashariki ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, maeneo ambayo katika miaka ya karibuni yaliharibiwa na fujo na vuruguu, na kusababisha halaiki ya raia kungo’lewa makazi na kuelekea kwenye maeneo mengine walipopatiwa uhamisho wa muda.~

Hapa na Pale

Vikosi vya Ulinzi Amani vya UM katika JKK (MONUC), vikisaidiwa na helikopta za vita Ijumaa walishambulia wafuasi wa kundi la waasi wa CNDP kwenye mji uliopo eneo la mashariki, kilomita 60 kutoka mji wa Goma. Waasi hao walikuwa wanaelekea jimbo la Kivu Kaskazini kwa madhumuni ya kuuteka mji baada ya kutangaza kabla dhamira yao hiyo. Shambulio la vikosi vya MONUC liliwalazimisha kurudi nyuma na kukatiza lengo lao.~~

Waathiriwa walionajisiwa kimabavu wadai kurejeshewa haki katika JKK

Hivi karibuni Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), likijumuika na wanaharakati wa Marekani wanaogombania haki za wanawake wanaowakilisha kundi linalojulikana kwa umaarufu kama Jumuiya ya V-Day, walitayarisha warsha mbili muhimu za pamoja, katika miji ya Goma na Bukavu. Kauli mbiu ya mkusanyiko huo ilikuwa na mada isemayo “Wanawake Wavunja Ukimya na Miko” – ambapo kwa mara ya kwanza, kihistoria, wale wanawake walionusurika na janga ovu la kunajisiwa kimabavu, walipata fursa ya kujieleza, hadharani, mbele ya kadamnasi ya raia, juu ya mateso waliopata kutokana na udhalilishaji wa kijinsia.

UNIFEM inasema serikali na mashirika ya kimataifa yanawajibika kukamilisha ahadi za MDGs

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Wanawake (UNIFEM) kwenye ripoti iliowakilishwa rasmi kwenye Makao Makuu ya UM Alkhamisi ya leo, ilieleza kwamba usawa wa kijinsia hauwezi kukamilishwa kama ilivyopendekezwa na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) bila ya kuwepo uwajibikaji wa nguvu utakaosaidia kukamilisha ahadi zilizotolewa kusukuma mbele maendeleo ya wanawake.

Mifumko ya bei yashadidia njaa ulimwenguni kwa watu milioni 75

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeripoti ya kwamba watu milioni 75 ziada wameingizwa rasmi kwenye safu za watu wenye njaa sana duniani, hali ambayo inazorotisha na kuchafua zile juhudi za kupunguza njaa kwa nusu katika 2015, kama ilivyopendekezwa na lengo la awali la Maendeleo ya Milenia (MDGs).

Tume juu ya tukio la Beit Hanoun yawakilisha ripoti katika HRC

Hii leo mjini Geneva kwenye ukumbi wa Baraza la Haki za Binadamu (HRC), Askofu Mkuu wa Afrika Kusini Desmond Tutu aliwakilisha ripoti ya mwisho juu ya matokeo ya uchunguzi waliofanya tume aliyoiongoza, ya hadhi ya juu, kuhusu shambulio la mwezi Novemba 2006 kwenye eneo la Wafalastina liliokaliwa kimabavu na Israel la Beit Hanoun, liliopo katika Tarafa ya Ghaza, ambapo raia 19 waliuawa na mizinga ya wanajeshi wa Israel.

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuunga mkono huduma za kusaidia watoto maskini 155,000, wanaohudhuria skuli za msingi 883, kupata mlo wa kila siku kwenye jimbo la Toliara nchini Bukini. Krystyna Bednarska, mwakilishi mkazi wa UNICEF-Bukini, alisema mradi huu utaiwezesha Bukini kukamilisha, kwa wakati, lile lengo la MDGs la kuwapatia watoto wote, wanaume na wanawake, ilimu ya msingi. Serikali ya Bukini imeshachangisha dola milioni 2.4 kuhudumia mradi huo.

Raisi mpya wa BK ahimiza demokrasia ihuishwe katika UM

Raisi mpya wa Baraza Kuu la UM, Miguel D’Escoto Brockmann, aliyekuwa Waziri wa Nchi za Nje wa Nicaragua, jana jioni alifungua rasmi kwenye Makao Makuu ya UM kikao cha 63 kinachojumuisha Mataifa Wanachama 192 kutoka kila pembe ya dunia, ambapo wajumbe wao hukusanyika kila mwaka, kuanzia mwezi Septemba hadi Disemba, kuzingatia masuala yote muhimu ya kimataifa, na kuchukua maamuzi kwa kulingana na kanuni za Mkataba wa UM.