Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuunga mkono huduma za kusaidia watoto maskini 155,000, wanaohudhuria skuli za msingi 883, kupata mlo wa kila siku kwenye jimbo la Toliara nchini Bukini. Krystyna Bednarska, mwakilishi mkazi wa UNICEF-Bukini, alisema mradi huu utaiwezesha Bukini kukamilisha, kwa wakati, lile lengo la MDGs la kuwapatia watoto wote, wanaume na wanawake, ilimu ya msingi. Serikali ya Bukini imeshachangisha dola milioni 2.4 kuhudumia mradi huo.

Ripoti ya KM juu ya mzozo wa mipaka kati ya Djibouti na Eritrea, ilizingatiwa katika Baraza la Usalama na wajumbe wa kimataifa. Ripoti ilijumuisha matokeo ya ziara ya tume ya uchunguzi iliotembelea mataifa ya Djibouti na Eritrea hivi karibuni, ikiwa katika juhudi za kimataifa kuudhibiti mvutano uliojiri kati ya mataifa hayo mawili juu ya umiliki wa mipaka yao. Ripoti ilisema wenye madaraka Eritrea walikataa kukutana nao, ikimaanisha matokeo ya ripoti yanawakilisha maoni ya upande mmoja tu, yaani Djibouti. Kwa muda mrefu, mataifa ya Djibouti na Eritrea yaliweza kuwa na uhusiano mzuri wa kijirani, mpaka mwezi Juni mwaka huu, baada ya kuzuka mzozo wa mipaka na uhusiano huo ukachukua sura tofauti. Tume imetahadharisha ya kwamba pindi walimwengu watashindwa kukabiliana na tatizo la mpaka wa Djibouti-Eritrea, kwa wakati, na kikamilifu, kuna hatari ya kuenea athari mbaya dhidi ya utulivu na amani, hali ambayo huenda ikalivaa eneo zima la Pembe ya Afrika na kuhatarisha usalama wa kimataifa.