Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waathiriwa walionajisiwa kimabavu wadai kurejeshewa haki katika JKK

Waathiriwa walionajisiwa kimabavu wadai kurejeshewa haki katika JKK

Hivi karibuni Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), likijumuika na wanaharakati wa Marekani wanaogombania haki za wanawake wanaowakilisha kundi linalojulikana kwa umaarufu kama Jumuiya ya V-Day, walitayarisha warsha mbili muhimu za pamoja, katika miji ya Goma na Bukavu. Kauli mbiu ya mkusanyiko huo ilikuwa na mada isemayo “Wanawake Wavunja Ukimya na Miko” – ambapo kwa mara ya kwanza, kihistoria, wale wanawake walionusurika na janga ovu la kunajisiwa kimabavu, walipata fursa ya kujieleza, hadharani, mbele ya kadamnasi ya raia, juu ya mateso waliopata kutokana na udhalilishaji wa kijinsia.

Taarifa za UM zimethibitisha kwamba vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, vya kunajisi wanawake na watoto wa kike kimabavu, ulianza kutumiwa tangu 1996 na makundi yanayoshiriki kwenye mapigano katika JKK, kwa madhumuni ya kutesa na kufedhehesha, kwa makusudi, waathiriwa wa jinai hiyo, kimwili na kiakili, wao na aila zao na kutumia jinai hiyo kama silaha ya vita. UM unakadiria tangu mapigano na uhasama kuzuka nchini humo katika miaka 12 iliopita, watoto wa kike na wanawake 200,000 walinajisiwa kimabavu katika JKK.

Mwandishi habari wa Redio ya UM, Jean-Pierre Ramazani alipata fursa ya kumhoji, kwa njia ya simu, mmoja ya waathiriwa alioshiriki kwenye warsha ulioandaliwa bia na UNICEF na Jumuiya ya V-Day. Bibi huyo anaitwa Valentine Faida Balezi. Mahojiano yaliendeshwa kwa Kiswahili kinachotumia lahaja ya Kikongo.

Sikiliza mahojiano kamili kwenye idhaa ya mtandao.