Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Baraza la Usalama linasailia operesheni za UNAMID Darfur

Ijumatatu wajumbe wa Baraza la Usalama walionyesha kuwepo mfarakano na mgawanyika kuhusu suala la kuongeza muda wa vikosi vya mchanganyiko vya Umoja wa Mataifa/Umoja wa Afrika kwa Darfur, yaani vikosi vya UNAMID. Mataifa ya Afrika Kusini na Libya yalipendekeza kuwepo kibwagizo maalumu kwenye azimio la kuongeza muda wa operesheni za vikosi vya UNAMID, kifungu kinachoitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Halaiki (ICC) kuakhirisha mashitaka dhidi ya Raisi Omar Al Bashir wa Sudan.

UNCTAD imewasilisha ripoti mpya ya biashara na maendeleo duniani

Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) limewasilisha Geneva takwimu mpya kwa 2008 juu ya biashara ya kimataifa. Takwimu za UNCTAD zimethibitisha katika 2007 biashara baina ya nchi zinazoendelea ziliongezeka. Lakini ripoti pia ilitilia mkazo nchi ziliotawala kwenye soko la kimataifa, hasa kwenye shughuli za kusafirisha bidhaa nje na kwenye biashara za huduma zilikuwa ni mataifa yenye maendeleo ya viwandani. Asilimia 70 ya jumla ya pato la ulimwengu katika 2007 iliwakilishwa katika nchi zenye maendeleo ya viwandani licha ya kuwa idadi yao ni asilimia 15 ya umma wa kimataifa.

Hapa na pale

Shirika la Kimataifa juu ya Uhamaji (IMO) limeanzisha miradi maalumu ya kuwapatia raia wa nchi za Afrika karibu na Ghuba ya Aden mafunzo maalumu kuhusu hatari ya safari za magendo zinazokwenda kinyume na sheria. Imweripotiwa na IMO kwamba katika 2007 watu 1,400 kutokea Ethiopia na Usomali, waliochukua safari za magendo kuvuka Ghuba ya Aden walifariki ama kwa kuzama au kuuawa na majambazi waliowatorosha kimagendo. Wawakilishi wa IMO wapo Addis Ababa, Ethiopia wakijaribu kushirikiana na jumuiya za kiraia, pamoja na viongozi wa kidini kwa lengo la kuwapatia mafunzo wale wenye dhamira ya kuhama kimagendo kwenda Yemen juu ya hatari ya kuvuka Ghuba ya Aden bila ya vibali vinavyotakikana, na kuwaelezea hatari ya safari hizo na taratibu zinazotakikana kuchukuliwa kijiepusha na matatizo kama hayo katika siku zijazo.

ECOSOC imekamilisha kikao cha mwaka

Baraza la UM juu ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) Ijumaa lilikamilisha mkutano wa mwaka, wa msingi, uliofanyika Makao Makuu ya UM mjini New York. Mkutano ulichukua karibu mwezi mmoja, na kwa mara ya kwanza wajumbe waliokusanyika mkutanoni walifanyisha kikao maalumu cha Halmashauri ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiufundi (DCF).

Jamii ya kimataifa inahimizwa na KM kuimarisha ari ya Olimpiki

KM wa UM Ban Ki-moon amewasilisha risala maalumu, kwa kupitia njia ya vidio kuhusu Michezo ya Olimpiki ya mwaka huu itakayofanyika Beijing, Uchina. Risala imependekeza vita isitishwe kote duniani katika kipindi chote michezo ya Olimpiki inafanyika Uchina, kuanzia mwezi Agosti. Kwa mujibu wa risala ya KM, malengo ya maadili ya kimsingi ya Michezo ya Olimpiki hufanana sawa na yale ya UM: hasa katika kukuza mafahamiano na kuhishimiana kati ya wanadamu; na katika majukumu ya kuandalia umma wa kimataifa fursa ya kufanikiwa, kwa usawa, kimaendeleo kwa kufuata taratibu na sheria; na muhimu ya yote katika kuimarisha utulivu na amani kwa wote.

Mkuu wa WTO ana matumaini majadiliano yanaingia sura ya kuvutia

Pascal Lamy, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) Ijumatatu aliwaambia waliohudhuria kikao kisio rasmi, Geneva, cha Kamati ya Mapatano ya Biashara ya kwamba ana matumaini kuhusu mwelekeo wa kimawazo kati ya nchi wanachama juu ya suluhu ya zile mada zilizozusha mvutano kwenye majadiliano. Alisema wajumbe waliohudhuria vikao kadha vya mkutano wameonyesha moyo wa kutaka kupatikane suluhu ya kuridhsiha, kwa wote, na hiyo ni ishara nzuri ya kukwamua vizingiti vya hapa na pale vinavyozorotisha majadiloiano, baadhi ya wakati, hususan katika masuala yanayohusu biashara ya kilimo, mathalan, idadi ya kikomo cha ndizi kuuzwa na yale mataifa yenye kuzalisha mavuno hayo.

Hapa na Pale

Ijumatatu, Baraza Kuu la UM limepitisha, kwa kauli moja, pendekezo la KM la kumteua Jaji Navanethem Pillay wa Afrika Kusini kuwa Kamishna Mkuu mpya wa UM juu ya Haki za Binadamu, kwa muda wa miaka minne, kuanzia Septemba 2008. ~~

ITU imeanzisha mfumo mpya kuokoa watu kwa simu ya mkononi

Shirika la Kimataifa juu ya Mawasiliano ya Simu (ITU) limewasilisha utaratibu mpya wa matumizi ya simu za mkononi, uliokusudiwa kusaidia wafanyakazi wanaoshughulikia huduma za kuokoa watu kupata uwezo wa kutambua haraka nani wa kuarifiwa kwanza, kwa jamaa wa waathiriwa wa maafa au hali ya dharura. ~

BU inazingatia "marekibisho" kwenye operesheni za UNMIK Kosovo

Baraza la Usalama lilikutana asubuhi kuzingatia ripoti mpya ya KM juu ya operesheni za Shirika la Usimamizi wa Utawala wa Muda Kosovo (UNMIK). Katika ripoti KM amesisitiza marekibisho lazima yafanyike kwenye kazi za UNMIK "yatakayokuwa na uzito mkuu, ili kukabiliana na hali halisi mpya" iliotanda kwa sasa katika Kosovo. Ripoti ilisema uwezo wa UNMIK kuendeleza shughuli zake kama ilivyodhaminiwa na Baraza la Usalama umepwelewa kwa sababu ya "vizingiti kadha vilivyojiri kutokana na hatua zilizochukuliwa na wenye madaraka katika Pristina na pia Waserb wa Kosovo."