Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

BU inazingatia "marekibisho" kwenye operesheni za UNMIK Kosovo

BU inazingatia "marekibisho" kwenye operesheni za UNMIK Kosovo

Baraza la Usalama lilikutana asubuhi kuzingatia ripoti mpya ya KM juu ya operesheni za Shirika la Usimamizi wa Utawala wa Muda Kosovo (UNMIK). Katika ripoti KM amesisitiza marekibisho lazima yafanyike kwenye kazi za UNMIK "yatakayokuwa na uzito mkuu, ili kukabiliana na hali halisi mpya" iliotanda kwa sasa katika Kosovo. Ripoti ilisema uwezo wa UNMIK kuendeleza shughuli zake kama ilivyodhaminiwa na Baraza la Usalama umepwelewa kwa sababu ya "vizingiti kadha vilivyojiri kutokana na hatua zilizochukuliwa na wenye madaraka katika Pristina na pia Waserb wa Kosovo."

Kwa hivyo, iliongeza kusema ripoti, KM ameamua kufanya marekibisho katika shughuli za UNMIK, na "ameamuru UNMIK ishirikiane, kikamilifu, kwenye huduma za utawala na zile taasisi nyengine ziliopo Kosovo za Umoja wa Ulaya (EU)". Kadhalika, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Kosovo, Lamberto Zannier alihutubia Baraza la Usalama kwa mara ya kwanza tangu alipokabidhiwa madaraka na kuwasilisha, kwa kina, maelezo juu ya hali halisi katika Kosovo.