Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ijumatatu, Baraza Kuu la UM limepitisha, kwa kauli moja, pendekezo la KM la kumteua Jaji Navanethem Pillay wa Afrika Kusini kuwa Kamishna Mkuu mpya wa UM juu ya Haki za Binadamu, kwa muda wa miaka minne, kuanzia Septemba 2008. ~~

Baraza la Usalama alasiri limekutana kwenye kikao cha faragha kushauriana kuhusu operesheni za ulinzi wa amani za vikosi vya mchanganyiko vya UA/UM kwa Darfur (UNAMID). Baadaye katika wiki Baraza linatarajiwa kupitisha azimio jipya kuhusu shughuli za UNAMID katika Darfur.

Staffan de Mistura, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Iraq ameshtumu vikali mashambulio ya mabomu yaliotukia Ijumatatu kwenye miji ya Baghdad na Kirkuk ambapo darzeni za raia waliuawa, na mamia ziada ya raia kujeruhiwa, tukio liliofuatia shambulio jengine maututi la Ijumapili katika mji wa Mada'in ambapo watu saba walipigwa risasi na kuuawa. Mistura aliwanasihi raia wa Iraq kuungana na kujikinga na wale waovu walionuia kuwasha tena moto wa fujo za kimadhehebu na kikabila nchini.

KM Ban Ki-moon ameshtumu pia mashambulio ya mabomu Ijumapili katika Istanbul, ambapo iliripotiwa raia 16 waliuawa na wingi wengineo kujeruhiwa. Kadhalika KM alilaani vikali mfululizo wa mabomu mengine yaliotukia India Ijumapili, hali kadhalika, yalioua na kujeruihi raia kadha. Alisisitiza kwamba hakuna sababu za kuridhisha wala masikitiko yanayomkumba mwanadamu yenye kuhalalisha vitendo vya kigaidi kama hivi, na ametahadharisha waathiriwa kuonyesha uvumilivu na kutochochewa na vitendo katili vya uchokozi vya kigaidi.